Zuberi Katwila aipigia hesabu kali Yanga
Muktasari:
- Katwila aliliambia Mwanaspoti, wakati maandalizi yao yanaendelea, benchi lake linatafuta mpango sahihi wa kudhibiti idara mbili za Yanga kwenye mchezo huo.
GEITA Gold inaendelea na maandalizi ikiwasubiri Yanga kumaliza ratiba ya mechi za kimataifa. Sasa kocha wa kikosi hicho, Zuberi Katwila amefunguka hesabu zake kuelekea mchezo huo dhidi ya mabingwa hao.
Katwila aliliambia Mwanaspoti, wakati maandalizi yao yanaendelea, benchi lake linatafuta mpango sahihi wa kudhibiti idara mbili za Yanga kwenye mchezo huo.
Katwila amesema, wakati wanakutana na Yanga lazima kikosi chake kijue namna ya kucheza kwa ubora, kwenye kuidhibiti safu ya kiungo ya Mabingwa hao ambayo ndio msingi wa ubora wao.
Kocha huyo amesema mbali na eneo la kiungo, pia kuna kazi ya kukabiliana na washambuliaji wa Yanga.
“Tunaendelea na maandalizi yetu lakini tunafahamu tunakwenda kucheza mechi ngumu nyingine sawa na ile tuliyocheza na Simba, hizi ni timu kubwa,” amesema Katwila.
“Unapokutana na timu bora kama hii lazima ujue namna ya kuwadhibiti eneo la kiungo, Yanga wako vizuri sana eneo la kati, hivyo tuna mkakati wa kuwanyima wasipate muda wa kutosha kumiliki mpira.
“Kule mbele nako wana watu bora sana ambao haitakiwi tufanye makosa, haya yote lazima tujipange nayo sasa.”
Aidha Katwila ameongeza kuwa, ana imani na safu yake ya ushambuliaji ina nguvu ya kuwalazimisha mabeki wa Yanga kufanya makosa, akimtanguliza mshambuliaji wa zamani wa mabingwa hao, Obbrey Chirwa.
Geita ambayo imecheza mechi tano mpaka sasa na kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, itakuwa mgeni wa Yanga Septemba 15, 2026 kwenye mechi sita itakazochezwa Uwanja wa KMC Complex ulioko Mwenge, Dar es Salaam.