Prime
Cheki wanasoka Kenya wenye mkwanja mrefu

Muktasari:
- Soka la kulipwa limeshika zaidi. Nyota wa mchezo huu wanavuna pesa nyingi kutokana na mauzo yao kutoka timu moja hadi nyingine pamoja na mishahara na bonasi za klabu zao.
HAKUNA ubishi kwa sasa soka ndiyo mchezo unaopendwa zaidi duniani. Ndiyo mchezo unaovuta hisia za wengi na ni moja ya michezo inayotengeneza pesa nyingi sana.
Soka la kulipwa limeshika zaidi. Nyota wa mchezo huu wanavuna pesa nyingi kutokana na mauzo yao kutoka timu moja hadi nyingine pamoja na mishahara na bonasi za klabu zao.
Ndiyo maana kwa sasa nyota wengi hasa kutoka Afrika wanajaribu bahati zao kwenye soka la kulipwa Ulaya na kwengine duniani kujitafutia riziki.
Mfano mzuri katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki, majirani zetu Kenya wana wanasoka wengi wanaosakata soka nchi mbalimbali duniani na wanatengeneza maisha yao kwa kulamba madili makubwa ya mikataba na mishahara.
Mwanaspoti linakuletea wanasoka 10 wenye mkwanja mrefu kutoka Kenya kwa mwaka 2025 wanaozidiana kwa utajiri kutokana na wanachokipata.
10. AYUB MASIKA (BIL 2.5)
Ayub Masika (32) ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars) na klabu ya Sabail ya Azerbaijan. Kwa miaka mingi amejijengea heshima kubwa katika ligi mbalimbali za Kimataifa zikiwemo Ubelgiji, England na China.
Pia ana dili nyingine za mkataba ya matangazo tofauti na anavyoingiza kwenye klabu yake na kumfanya kufikisha tajiri wa Dola1 milioni, zaidi ya Tsh2.5 bilioni na kuwa miongoni mwa wanasoka wa Kenya matajiri mwaka huu 2025.

9. ISMAEL ATHUMAN (BIL 2.8)
Beki wa kati ambaye ana uwezo wa kucheza pia nafasi ya kiungo mkabaji. Alizaliwa miaka 30 iliyopita, Maspalomas, Hispania na ameonyesha kipaji chake katika ligi mbalimbali za nchi hiyo akicheza timu za UD Las Palmas, Real Murcia, Merida AD alikotengeneza pesa kutokana na mikataba na mishahara.
Pia thamani yake ilipanda kutokana na kushiriki michezo ya timu ya taifa 'Harambee Stars' na mikataba ya matangazo na anakuwa miongoni kwa wanasoka matajiri Kenya akiwa na jumla ya Dola 1.1 milioni, zaidi ya Tsh2.8 bilioni.
8. DAVID OCHIENG (BIL 3.1)
David 'Cheche' Ochieng (32). Ni beki wa kati wa klabu ya Ligi Kuu Kenya (FKF PL), Kenya Police FC na Harambee Stars. Kwa miaka mingi nyota huyu alikuwa akisaka maisha ughaibuni katika ligi mbalimbali zikiwamo za Saudia Arabia, Uswisi na Marekani.
Nyota huyu anakadiriwa kuwa na utajiri wa takribani Dola 1.2 milioni, sawa na Tsh3.1 bilioni na kuwa mmoja wa mabeki tajiri zaidi katika historia ya soka la Kenya.

7. LAWRENCE OLUM (BIL 3.9)
Olum (40) ni beki na kiungo wa kati wa zamani wa Harambee Stars. Alipata mafanikio makubwa kisoka akiwa Ligi Kuu Marekani (MLS) akizichezea Portland Timbers na Sporting Kansas City, akivuna mishahara na bonasi za kutosha.
Utajiri wake unakadiriwa kufikia takriban Dola 1.5 milioni 1.5, sawa na Tsh3.9 bilioni.
6. ARNOLD ORIGI (BIL 4.6)
Origi (41) ndie kipa pekee kutoka Kenya anayecheza soka Ulaya kwa zaidi ya miaka 15, akicheza katika nchi za Norway, Uswizi na Finland.
Amepita katika klabu za Hareid IL, Moss, Fredrikstand, Kongsvinger, Hodd, Lillestrom za Norway, Ostersund ya Sweden na Helsinki IFK ya Finland na Mathare United na Tusker FC za Kenya.
Kwa sasa nyota huyo hulia kimvulini tu kutokana na kazi kubwa ya kugeuza kipaji chake kuwa fursa ilivyomsaidia kupata mkwanja mrefu akiwa na utajiri wa Dola1.8 milioni, sawa na Tsh4.6 bilioni.
5. JAMAL MOHAMMED (BIL 5.2)
Jamal Mohammed (40 huyu alikuwa ni kiungo mahiri ambaye amechezea klabu za Kenya, Oman na Mashariki ya Kati) ambako ametengeneza pesa nyingi katika safari yake hiyo ya kisoka.
Jamal pia alitengeneza pesa kutokana na ushawishi wake yani mvuto aliokuwa nao na aliingia mikataba na kampuni mbalimbali za matangazo.
Utajiri wake unakadiriwa ni wa Dola 2 milioni, sawa na Tsh5.2 bilioni na sasa katundika daruga.
4. PATRICK OSIAKO (BIL 5.2)
Patrick Osiako (38) alifurahia maisha yake ya soka kwa muda mrefu na yenye mafanikio, akicheza katika ligi za Uswizi, Israel, na Azerbaijan na kuvuna pesa, huku pia akiwekeza kwa ajili ya maisha baada ya soka.
Baada ya kustaafu soka Osiako bado anaendelea kupata mapato akimiliki biashara mbalimbali na mafanikio hayo yanamfanya kuwa mfano wa kuigwa kwa wanasoka wajao.
Utajiri wake ni wa Dola 2 milioni, sawa na Tsh5.2 bilioni.

3. MICHAEL OLUNGA (BIL 10.4)
Michael Olunga, nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Kenya. Amefanya makubwa katika soka la kimataifa, kwa sasa anacheza nchini Qatar katika klabu ya Al-Duhail SC, anapokea mshahara wa kila mwaka unaokadiriwa kufikia Dola 1 milioni zaidi ya Tsh1.5 bilioni.
Olunga aliweka historia ya kuwa Mkenya wa kwanza kufunga hat-trick kwenye Ligi Kuu ya Hispani (La Liga) alipokuwa akiichezea Girona aliyoiongoza kushinda mabao 6-0 dhidi ya Las Palmas akitumia dakika 22, Januari 13,2028.
Ubora wake umemfanya kupata mikataba yenye pesa ndefu mrefu na kujingenezea utajiri katika umri mdogo tu wa miaka 30.
Utajiri wake unakadiriwa kufikia Dola milioni 4, zaidi wa Tsh10.4 bilioni inayomfanya kuwa mmoja wa wanasoka wa thamani zaidi wa Kenya, akiendelea kuvunja rekodi na kuweka hatua mpya.

2. MACDONALD MARIGA (BIL 18)
Macdonald Mariga (37), kiungo mstaafu, alikuwa Mkenya wa kwanza kushinda UEFA Champions League mwaka 2010 akiwa na Inter Milan.
Kazi yake yenye mafanikio Italia, Uhispania na England ilimletea mamilioni ya pesa kutokana na mishahara na marupurupu.
Baada ya kustaafu, Mariga alibadilisha maisha na kuwekeza kwenye biashara na siasa ambayo ilimuongezea utajiri zaidi na kumfanya kuwa miongoni mwa wanasoka tajiri zaidi Kenya.
Akiwa na utajiri wa Dola 7 milioni, sawa na Tsh18 bilioni. Kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF).

1. VICTOR WANYAMA 35 Bilioni
Victor Wanyama (33) ndiye mwanasoka tajiri zaidi wa Kenya mwaka 2025 akiwa na utajiri wa Dola 13.9 milioni (zaidi ya Tsh35 bilioni).
Nyota huyu amewahi kuchezea Klabu mbalimbali zikiwemo Tottenham Hotspur, Southampton zinazoshiriki Ligi Kuu England na Celtic ya Scotland.
Wanyama amepata mamilioni ya mishahara na bonasi licha ya kutokuwa na klabu sasa baada ya kuondoka CF Montreal ya Ligi Kuu Marekani (MLS) anaendelea kula maisha kwa fedha nyingi ambazo amevuna kupitia soka.
Mafanikio yake ni pamoja na kuwa Mkenya wa kwanza kufunga bao katika UEFA Champions League na hivyo kuimarisha urithi wake.
Kando na soka, Wanyama pia amewekeza kwenye biashara na kujihakikishia mafanikio ya kifedha ya muda mrefu.