Kocha Man United atua Harambee Stars

Muktasari:
- Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), McCarthy, ambaye alikuwa kocha wa washambuliaji kwenye kikosi cha Manchester United ya England, atachukua mikoba ya kuinoa Harambee Stars, ambayo kwa sasa ipo chini ya kocha wa muda, Francis Kimanzi.
STRAIKA wa zamani wa timu ya soka ya Afrika Kusini, Benni McCarthy, anatarajiwa kutua Kenya mwishoni mwa wiki kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa ya nchi hiyo, Harambee Stars, inaripotiwa Nation Sport.
Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), McCarthy, ambaye alikuwa kocha wa washambuliaji kwenye kikosi cha Manchester United ya England, atachukua mikoba ya kuinoa Harambee Stars, ambayo kwa sasa ipo chini ya kocha wa muda, Francis Kimanzi.
McCarthy, ambaye aliifungia Bafana Bafana mabao 31 kwenye mechi za kimataifa, shughuli pevu inayokwenda kumkabili huko Kenya ni kukiongoza kikosi cha Harambee Stars kwenye mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Gabon, Machi 24 kwenye Uwanja wa Nyayo.
"Tuna kocha mpya, Benni McCarthy, ambaye atachukua timu na anatarajiwa kuwasili nchini kabla ya wiki haijamalizika. Yeye ni kocha aliyehitimu na tunaamini atasaidia kuiongoza timu ya taifa kuleta mafanikio," alisema afisa huyo wa FKF.

"Lengo letu ni kujenga timu nzuri itakayosaidia Kenya kurudi katika nyakati nzuri ikiwa ni pamoja na uteuzi mzuri wa wachezaji kwenye timu ya taifa."
Tofauti na makocha wa kigeni waliopita, McCarthy hatakuja na benchi lake la ufundi, badala yake, timu ya sasa ya makocha itabaki na itakuwa sehemu ya benchi la ufundi kumsaidia.
Kimanzi alikinoa kikosi cha Harambee Stars kama kocha wa muda alipochukua mikoba ya kocha mkuu, Mturuki Engin Firat, ambaye aliachia ngazi Desemba 11, 2024.
"Wakati huu, tumeweka kila kitu sawa, na maelezo ya makubaliano yatatolewa hivi karibuni, lakini yeye ni kocha wetu mpya, na tunatarajia atajenga timu inayoshindana," aliongeza afisa huyo wa FKF.
McCarthy, mwenye umri wa miaka 47, pia anatarajiwa kuhudhuria mechi ya mahasimu wawili kwenye Ligi ya Kenya, AFC Leopard na Gor Mahia zitakazochuana kwenye “Mashemeji derby”, Jumapili, Machi 3.
Baada ya kucheza michezo yake ya kimataifa katika nchi za Uganda na Afrika Kusini, Harambee Stars sasa itatumia uwanja wake wa nyumbani wa Nyayo katika mchezo huo dhidi ya Gabon, ikiwa ni sehemu pia ya majaribio ya uwanja huo ambao utatumika kwenye fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa ndani, Chan 2024.
Kenya imepangwa Kundi F kwenye mchakamchaka wa kufuzu Kombe la Dunia 2026, ambapo kwa sasa ikiwa inashika nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi tano katika mechi nne. Ivory Coast inaongoeza kundi hilo ikiwa na pointi 10, ikifuatiwa na Gabon (pointi tisa), Burundi (pointi saba), Gambia (pointi tatu), na Seychelles (pointi sifuri).
McCarthy aliwahi kuzichezea klabu za Ajax, Celta Vigo, FC Porto, Blackburn Rovers, West Ham, na Orlando Pirates. Pia alicheza michezo 79 kwa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, na kufunga mabao 31.

Kwa upande wa ukocha, McCarthy alizonoa Cape Town City, Amazulu, na pia alikuwa kocha msaidizi wa Sint-Truiden. Kati ya 2020 na 2024, McCarthy alikuwa kocha wa kikosi cha kwanza cha Man United, akisimamia washambuliaji alipofanya kazi chini ya Erik ten Hag. Kwa uzoefu wake mkubwa, FKF inaamini McCarthy atabadilisha hali ya mambo Harambee Stars.