Mfahamu Harold Ndege CEO mpya FKF

Muktasari:
- Kenya inaendesha Ligi Kuu katika mfumo unaoifanya ijiendeshe yenyewe kupitia chombo maalumu kinachoitwa FKF-PL na hapa ndipo alipo Harold Ndege, mtendaji mkuu mpya wa muhimili huo.
SHIRIKISHO la Soka Kenya (FKF) lina uongozi mpya, lakini baada ya kuingia madarakani mambo mengi katika soka nchini humo yamebadilika. Yapo mabadiliko kuanzia ngazi ya uongozi hadi katika uendeshaji wa mashindano mbalimbali yaliyopo chini ya shirikisho hilo.
Kenya inaendesha Ligi Kuu katika mfumo unaoifanya ijiendeshe yenyewe kupitia chombo maalumu kinachoitwa FKF-PL na hapa ndipo alipo Harold Ndege, mtendaji mkuu mpya wa muhimili huo.
Ndege ni nani? Huyu ni mwanasoka aliyewahi kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu Kenya na makombe mawili ya Cecafa akiwa na Kenya Breweries (sasa Tusker FC) na pia aliichezea timu ya taifa (Harambee Stars) mara sita.
Hata hivyo, Ndege hataki kutambulika pekee kwa mafanikio yake uwanjani, badala yake mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 44 anataka kuacha alama ya kudumu kwa kuleta mchango mkubwa katika biashara ya soka nchini Kenya.
“Nataka kuimarisha tasnia ya soka ya Kenya kibiashara, ambapo kila klabu inaweza kuzalisha mapato yake yenyewe. Kuhakikisha wachezaji, makocha, mawakala, waamuzi na washika dau wengine wanapata maisha bora,” anasema Ndege, CEO mpya wa FKF aliyetambulishwa hivi karibuni katika mahojiano na Nation Sport.
Mtendaji huyo alikamata nafasi hiyo Ijumaa baada ya kupitishwa kwa uteuzi wake na Kamati Kuu ya Utendaji ya FKF akichukua nafasi ya Patrick Korir aliyekuwa msimamizi wa mpito tangu Oktoba 2024 kujiuzulu mwezi huu.
Dennis Gicheru, aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Wazito FC, Collins Bob Otieno na Sarah Migwi walikuwa pia katika orodha ya waliokuwa wanachuana kuwania nafasi hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa FKF anasimamia shughuli za kila siku za shirikisho akiwa na lengo kuu la usimamizi bora wa soka, kifedha na ufanisi wa kiutendaji.
Ingawa Ndege alishindwa kuficha furaha yake kuhusu nafasi mpya, alikubali changamoto zilizopo.
Ndege ambaye ana Shahada ya Uzamili wa Fedha kutoka Taasisi ya Wataalamu wa Fedha ya India na Shahada ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Karnataka nchini India anasisitiza kuwa yuko tayari kwa kazi hiyo.
“Haitakuwa safari rahisi, bali ya milima na mabonde. Tumejua changamoto lakini tunalo suluhisho chini ya uongozi wa rais wetu Hussein Mohammed,” anasema Ndege
UZOEFU
Mchezaji huyo wa zamani wa Kenya, ambaye alifanya kazi katika sekta ya umma na binafsi, aliongoza sekretarieti ya Hussein katika kampeni ya urais wa FKF.
Wakati wa uchaguzi wa FKF 2020, alikuwa kama mgombea mwenza wa Herbert Mwachiro ambaye aligombea urais.
Amekuwa akizungumzia uwazi na usimamizi katika soka la Kenya, akiandika makala kadhaa katika Nation miaka ya nyuma.
Katika makala mojawapo mwaka jana iliyoitwa "Mabadiliko katika uongozi wa soka la Kenya yalikuwa ya muda mrefu" Ndege aliandika: “Bila kusema mengi, utawala wa sasa wa FKF una tabia ya kushindana katika uhalifu. Mazingira kama haya hayawezi kuendelea kutambua na kukuza vipaji. Pia, hayavutii mashabiki na wawekezaji.”
Ndege aliyezaliwa na kukulia katika Estate ya Kariobangi mjini Nairobi anasema alibebwa katika soka na binamu yake, Zacchaeus Omondi ambaye alikuwa mchezaji wa Tusker akicheza kama mshambuliaji.
Chini ya maelekezo ya kocha Jacob “Ghost” Mulee, beki huyo alisaini mkataba wake wa kwanza na Tusker 1999, mwaka ambao Tusker walitwaa taji la FKF-PL ambalo walilitetea pia 2000.
Pamoja na Mulee, Tusker walishinda Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) 2000 na 2001.
Ndege ambaye aliacha kucheza soka 2005 alichezea mechi sita za kimataifa 2000 chini ya Mulee na aliwahi kuchezea Klabu ya Vascos Sports nchini India katika Ligi Kuu wakati alipokuwa akisoma nchini humo.
“Kwa kuwa nilikuwa mchezaji wa soka katika viwango vya klabu na timu ya taifa, naielewa vyema tasnia ya soka. Nina uzoefu, ujuzi na rekodi nzuri kwa kazi hii,” anasema Ndege.
UONGOZI
Mbali na kuleta mabadiliko katika biashara ya soka ya Kenya, Ndege anaahidi kuhakikisha utekelezaji wa ahadi ya Hussein, ambayo inajumuisha maendeleo ya miundombinu, kupanga upya utawala ndani ya FKF, uendeshaji kidijitali shughuli na kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau.
“Nilisoma ripoti (ya Kamati Maalumu ya Uhamisho ya FKF). Kilichojitokeza ni kwamba tunahitaji kupata wafanyakazi wenye ujuzi wa kufanya kazi katika shirikisho. Tunahitaji kubadilisha thamani ya shirikisho kwa sababu kama wafanyakazi hawatafuata maadili sahihi, basi ubora wa huduma kwa wadau utakuwa mdogo,” anasema katibu mkuu huyo wa Chama cha Wachezaji wa Soka Kenya.
Pia ni mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Ustawi wa Wachezaji wa Soka wa Kenya.
Anasema wafanyakazi wa shirikisho watachunguzwa kulingana na viashiria muhimu vya utendaji ili kuongeza ufanisi.
“Harold Ndege ana kazi kubwa mbele yake na tunafurahi kumaliza mchakato huu,” anasema Hussein.
“Uzoefu wake katika utawala wa soka na usimamizi utakuwa muhimu katika kuongoza FKF mbele.”