Amorim kumpa nafasi Bukayo Saka mpya

Muktasari:
- Man United inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu, huku matumaini pekee ya kunyakua ubingwa kwa msimu huu yapo kwenye michuano ya Europa League, ambapo imefika hatua ya robo fainali.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim ameripotiwa kwamba yupo kwenye mipango ya kumpa nafasi ya kucheza kinda wa kikosi hicho cha Old Trafford ambaye analinganishwa kiuchezaji na winga wa Arsenal, Bukayo Saka.
Man United inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu, huku matumaini pekee ya kunyakua ubingwa kwa msimu huu yapo kwenye michuano ya Europa League, ambapo imefika hatua ya robo fainali.
Katika kuelekea mwisho wa msimu, kocha Amorim anafikiria kutoa nafasi kwa wachezaji makinda ili kufahamu ukubwa wa kikosi chake kitakachokuwa msimu ujao endapo kama hakutakuwa na pesa za kutosha za kusajili wakali wapya.
Mshambuliaji kinda Chido Obi ameshapewa nafasi ya kucheza, akitumika kwenye mechi nne alizotokea benchini tangu alipojiunga na Man United akitokea Arsenal, wakati Harry Amass naye alitokea benchini kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Leicester City kabla ya mapumziko ya ligi kupisha mechi za kimataifa.
Na sasa zamu ya kucheza inaweza kuhamia kwa kinda wa miaka 17, Bendito Mantato, ambaye amekuwa akiitwa Bukayo Saka mpya.
Ripoti zinafichua kwamba kocha wa Man United amepanga kumjumuisha winga huyo kwenye mpango wa kikosi chake cha kwanza baada ya kufunga mabao saba katika mechi 13 akiwa na kikosi cha U18 msimu huu, wakati alifunga pia bao la ushindi kwenye Kombe la FA la vijana katika mechi ya robo fainali ya ushindi dhidi ya Arsenal.
Mantato amekuwa akifanya mazoezi kwenye kikosi cha kwanza cha Man United, wakati mastaa wengine wa timu hiyo wakiwa kwenye majukumu ya soka la kimataifa, ambapo aliungana na makinda wenzake, Obi, Amass, Reece Munro, Godwill Kukonki na Jim Thwaites, ambao wanaonekana kumkosha kocha Amorim.
Winga huyo wa kulia, Mantato amekuwa akitumika kama beki wa kushoto kwenye kikosi cha vijana cha Man United, huku uwezo wake wa kucheza beki na winga ndicho kitu kinachomfanya kocha Amorim aamini ataweza kufiti katika mfumo wake wa 3-4-3.
Kwenye nafasi hiyo, kinda huyo atakuwa na kazi ya kushindania nafasi na wachezaji Diogo Dalot, Noussair Mazraoui na Patrick Dorgu.