Arsenal kuvuna mkwanja, ikiichapa Real Madrid

Muktasari:
- Goal inaripoti kwamba Arsenal inatarajiwa kupokea kiasi kikubwa cha fedha kutokana na kiwango chao katika Ligi ya Mabingwa, na mapato yao yanatarajiwa kuzidi Pauni 100 milioni.
LONDON, ENGLAND: MBALI ya kuwapa furaha mashabiki wao, tovuti ya Goal.com imefichua kwamba Arsenal inaweza kupata faida kubwa ya fedha katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa itaishinda Real Madrid na kufuzu nusu fainali.
Goal inaripoti kwamba Arsenal inatarajiwa kupokea kiasi kikubwa cha fedha kutokana na kiwango chao katika Ligi ya Mabingwa, na mapato yao yanatarajiwa kuzidi Pauni 100 milioni.
Timu hiyo ya kaskazini mwa London itafaidika na mfumo mpya wa ugawaji wa zawadi wa UEFA, ambao unalenga zaidi kutoa pesa mbali ya zawadi.
Kama sehemu ya mageuzi makubwa ya mashindano yake ya klabu, UEFA imebadilisha kwa kiasi kikubwa jinsi mapato ya Ligi ya Mabingwa yanavyogawiwa.
Shirikisho hilo limeweka utaratibu wa kuzipa zawadi timu kutokana na mafanikio ya uwanjani, maana yake ni kwamba timu sasa zinapata bonasi kubwa kwa kushinda mechi, kushika nafasi nzuri kwenye mfumo mpya wa ligi ulioanza msimu huu na kufika kwenye raundi za 16 bora.
Moja ya mabadiliko makubwa ni ongezeko la malipo ya awali kwa timu zilizofuzu kucheza hatua ya ligi ambapo kila mojawapo ilipokea Euro 18.6 milioni kabla ya kucheza mechi yoyote.
Mbali ya pesa hizi, timu pia zilipata pesa kutokana na nafasi zilizomaliza katika msimamo ambapo kwa upande wa Liverpool iliyokuwa kinara ilikunja Euro 10.6 milioni wakati timu iliyoshika mkia ikipata Euro 300,000.
Vilevile kwa timu ambazo zilimaliza hatua ya ligi kwa nafasi za juu na zikafanikiwa kutinga 16 bora Uefa ilitoa bonasi za ziada kwao ya Euro 2 milioni.
Pesa ambazo Uefa imeziweka kwa msimu huu zinaonekana kuwa kubwa zaidi na Man City ambayo iliondoshwa katika 16 bora imejipatia Pauni 64 milioni kiasi ambacho ni kikubwa zaidi ukilinganisha na msimu uliopita.
Vilevile Aston Villa iliyotinga robo fainali, tayari imeshajihakikishia kupata Pauni 71 milioni na ikiwa itaendelea inaweza kuvuna zaidi.
Hii ndio inaiweka Arsenal katika nafasi hiyo ya kupata karibia Pauni 100 milioni kutokana na kiwango chao katika michuano hii kwani ilimaliza nafasi nzuri katika msimamo wa ligi (ya tatu) hali ambayo iliwawezesha kupata bonasi kubwa zaidi na timu pekee ambayo inaweza kuifikia katika makusanyo ya pesa ni Barcelona iliyomaliza nafasi ya pili.