ATM YA WIKI: Mo Salah mkataba mpya, utajiri mpya

Muktasari:
- Mbali ya furaha ambayo mashabiki wa Liverpool wanatarajiwa kuipata kutokana na uwepo wa staa huyu, pia Salah mwenyewe anatarajiwa kupata pesa za kutosha na kuongeza utajiri zaidi.
MOJA kati ya habari kubwa kwa mashabiki wa Liverpool kwa mwezi huu ilikuwa ni kusaini mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamwezesha kusalia hadi mwaka 2027.
Mbali ya furaha ambayo mashabiki wa Liverpool wanatarajiwa kuipata kutokana na uwepo wa staa huyu, pia Salah mwenyewe anatarajiwa kupata pesa za kutosha na kuongeza utajiri zaidi.
Leo tumekuletea hapa, utajiri ambao anao na jinsi atakavyozidi kuongeza kupitia mkataba wake mpya.

ANAPIGAJE PESA
Kupitia mkataba wake mpya, Salah atalipwa takriban Pauni 500,000 kwa wiki ikiwa ni pamoja na mjumuisho wa bonasi.
Mbali ya mshahara fundi huyu pia amekunja karibia Pauni 10 milioni kama bonasi ya usajili, kiasi hicho cha pesa kimemfanya kufikisha utajiri unaokaribia Dola 90 milioni.
Mbali ya pesa hizo anazopata kama mshahara, Salah pia atapata pesa mwingine kutoka kampuni ya Adidas na inampa takriban Dola 10 milioni kila mwaka.
Pia ana mkataba na kampuni ya Vodafone na amekuwa balozi wa kampuni ya vinywaji ya Pepsi ambayo alisaini nao mkataba tangu mwaka 2016.
Katika kurasa zake za mitandao ya kijamii pia anapata pesa kutokana na matangazo ambayo yanawekwa huko.

MCHANGO KWA JAMII
Mwaka 2019 aliripotiwa kutoa kiasi cha Dola 3 milioni, kwenda kwa taasisi inayojishughulisha na masuala ya Kansa huko Oman, ili kwenda kusaidi mchakato wa kununua vifaa baada ya majambazi kuvamia na kuondoka na vifaa.
Pia ni balozi wa Shirika la Afya Duniani UNHCR, mbali na hilo Salah ni mmoja ya wadau wakubwa wa kusaidia watoto yatima na watu wasiojiweza, kupitia Mohamed Salah Charity Foundation.

NDINGA
Bentley Continental GT,Pauni 160,000
Bentley Bentayga,Pauni 170,000
Porsche 911 Turbo S,Pauni 180,000
Lamborghini Aventador,Pauni 270,000
Mercedes-Benz AMG GLE Coupe,Pauni 65,000
Mercedes-Benz SLS AMG Roadster, Pauni 175,000
Audi Q7, Pauni 67,000

MJENGO
Ana mijengo mitatu, miwili ipo nchini kwao Misri na moja ipo England katika Jiji la Liverpool. Kijumla nyumba zake zote zinakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 7 milioni.
Nyumba yake kubwa zaidi ni ile ya Liverpool ambayo ndani kuna sehemu ya kufanyia mazoezi.
MAISHA NA BATA
Yupo kwenye ndoa na mwanadada Maggi tangu Desemba17, 2013 na wamepata watoto wawili.
Kuhusu suala la bata jamaa sio mtu wa mambo hayo kabisa, muda mwingi wa mapumziko huwa anautumia kukaa na Familia yake.