Balaa la uwanja mpya, usajili mpya ni utata, mataji kuyeyuka

Muktasari:
- Man United, Jumanne ilitambulisha mwonekano wa uwanja wake mpya utakaokuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 100,000 wanaoketi, ambao kwa sasa umepachikwa jina la New Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imekiri kwamba inajiweka kwenye hatari ya kukosa ubingwa kwa miaka mingine mitano kutokana na kuwekeza pesa nyingi, Pauni 2 bilioni kwenye mradi wa ujenzi wa uwanja mpya.
Man United, Jumanne ilitambulisha mwonekano wa uwanja wake mpya utakaokuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 100,000 wanaoketi, ambao kwa sasa umepachikwa jina la New Trafford.
Lakini, utambulisho wa mradi huo umekuja ndani ya saa 24 tangu bilionea mmiliki wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe kudai kwamba klabu hiyo ingekuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kiuchumi hadi kufikia Krismasi iliyopita kama isingechukua hatua za kupunguza watu kazi.

Uamuzi huo wa kujenga uwanja mpya umeungwa mkono na nguli wa klabu hiyo, Sir Alex Ferguson.
Na kwenye hilo, mkurugenzi mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Omar Berrada anaamini kocha wa sasa Ruben Amorim ataendelea kuinoa timu hiyo hadi uwanja utakapokamilika 2030.
Lakini, bosi huyo aliulizwa kama ujenzi wa uwanja utaathiri uwekezaji kwenye timu ili kuifanya kuwa ya kiushindani ndani ya uwanja na hapo, Berrada alisema: "Hiyo ni hatari. Ni wazi ni kitu tunachotaka kukiepuka. Hatutaki kuzuia uwezo wetu wa kuwekeza kwenye timu ili kuendelea kushindana wakati huo tukiwa tunajenga uwanja mpya. Kuna njia nyingi za kuliwezesha hilo.
"Moja ya vitu hivyo ni kufupisha muda wa ujenzi kwamba tuwe na uwanja mpya ndani ya miaka mitano, huo ndio mpango wetu. Kwa wakati huo, wakati tukirudi kwenye nguvu yetu ya kiuchumi na kupata faida, tunaamini tunaweza kuwa na timu itakayokuwa ya ushindani."
Miamba ya Ligi Kuu England, Arsenal na Tottenham Hotspur yenyewe pia ilibadili viwanja vyao na kujenga vipya kwa kumbukumbu ya miaka ya hivi karibuni na kukabiliana na matokeo ya hovyo uwanjani.
Lakini, bosi Berrada aliongeza: "Faida kubwa iliyonayo klabu hii ni kwamba ina mashabiki wengi duniani, hivyo ina uwezo wa kuwa namba moja kwenye ishu ya kuzalisha mapato."
Man United itaanza ujenzi wa uwanja wao mpya mwaka huu, lakini matumaini ni kuanza kuutumia kwenye msimu wa 2030-31. Kundi la mashabiki la Manchester United Supporters Trust (MUST) lilibainisha muonekano wa uwanja huo mpya unavutia, lakini mradi wenyewe unaibua maswali mengi kuliko majibu. Kikosi cha Man United kwa sasa kinashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na kila kitu kipo wazi kwamba kikosi hicho kinahitaji maboresho makubwa ndani ya uwanja.
Berrada alisema: "Kama tutafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, tutakuwa na mapato ya kutosha ili kufanya uwekezaji zaidi kwenye timu."
VIWANJA VINAVYOINGIZA MASHABIKI WENGI DUNIANI
10. Estadio Azteca, 90,000
9. Wembley, 90,652
8. King Salman, 92,000
7. Lusail, 92,349
6. FNB, 94,736
5. Misr, 96,940
4. New Trafford, 100,000
3. Camp Nou, 105,000
2. Hassan II, 115,000
1. The Rungrado, 150,000