Barca yamweka Raphinha sokoni

Muktasari:
- Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil amekuwa na mchango mkubwa msimu huu katika kikosi hicho akiwa amefunga mabao 25 na kutoa asisti 15 katika La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA iko tayari kumuuza Raphinha dirisha la usajili la majira ya kiangazi ikiwa itapokea ofa ya Euro 80 milioni, taarifa zinaeleza kutoka Hispania.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil amekuwa na mchango mkubwa msimu huu katika kikosi hicho akiwa amefunga mabao 25 na kutoa asisti 15 katika La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Raphinha bado ana miaka miwili iliyosalia kwenye mkataba na Barcelona, na mazungumzo yameanza kuhusu mkataba mpya.
Hata hivyo, redio ya Catalunya inaripoti wawakilishi wake wanataka mshahara mkubwa kuliko ule ambao Barcelona iko tayari kulipa.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa Deco, mkurugenzi wa michezo wa Barca, amependekeza kumuuza Raphinha kwa timu ambayo inaweza kutimiza matakwa yake ya mshahara, ikiwa watapokea ofa ya kati ya Euro 80 hadi 90 milioni.
Pia inadaiwa Raphinha tayari amepokea ofa nono kutoka timu ya Ligi Kuu Saudi Arabia, lakini Mbarazili huyo hafikirii kuondoka labda baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia 2026. Bei ya Raphinha inadaiwa kuwa imefufua upya matamanio ya Arsenal na Chelsea, ambazo zilijaribu kumsajili kutoka Leeds United 2022.
Edu, aliyekuwa mkurugenzi wa michezo wa Arsenal wakati huo, alithibitisha kuwa alifanya mawasiliano na Deco, ambaye alikuwa wakala wa Raphinha kabla hajawa mkurugenzi wa michezo wa Barcelona.