Barcelona yalilia kupumzika La Liga

Muktasari:
- Katika mchezo wao wa mwisho Barcelona ilipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Atletico Madrid ambacho kilisababisha washushwe katika nafasi ya kwanza hadi ya pili.
BARCELONA, HISPANIA: KOCHA wa Barcelona, Hansi Flick, amekiri kuwa timu yake ilihitaji mapumziko katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kutokana na matokeo mabaya wanayoendelea kupata katika michezo ya hivi karibuni.
Katika mchezo wao wa mwisho Barcelona ilipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Atletico Madrid ambacho kilisababisha washushwe katika nafasi ya kwanza hadi ya pili.
Atletico ambayo inaongoza kwa pointi 41 katika msimamo wa La Liga huo ulikuwa ni mchezo wao wa 12 kushinda katika michuano yote.
Mapumziko ya majira ya baridi yanakuja kwa wakati mzuri kwa Barcelona ambao wanaweza kujipanga upya kabla ya kuteremka zaidi kutoka kileleni.
Hiki kinakuwa ni kipindi kigumu sana kwa Barcelona ambayo katika mechi saba zilizopita za La Liga imeshinda moja tu.
Flick anaamini huu utakuwa ni wakati sahihi kwao kupumzika na kujaribu kujenga upya kikosi ili warejee katika ubora mkubwa.
“Sasa ni mapumziko na nafikiri kila mtu anahitaji mapumziko haya. Baada ya mapumziko tutafanyia mazoezi na tutaonyesha ni jinsi gani tulivyo imara. Tumehuzunishwa sana na matokeo yetu ya hivi karibuni, na tuliumia pia kupoteza dhidi ya Atletico kwa sababu tulicheza vizuri, kwa sasa tutaenda kusherehekea Krismasi kisha tutaanza mazoezi tarehe 29 Desemba na kupambana kwa ajili ya nusu nyingine ya msimu.”
Katika vita ya ubingwa mbali ya Atletico, Real Madrid pia ipo nyuma yao kwa tofauti ya pointi moja ikiwa na michezo miwili mkononi kabla ya mchezo wao wa jana.
Baada ya kupumzika kwa wiki moja ili kusherehekea Krismasi, Barca itacheza mechi mbili dhidi ya Barbastro kwenye Kombe la Mfalme, kisha itacheza na Bilbao.