Bosi hana baya

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Erik ten Hag amesema “bosi hana baya” baada ya kikao na mmiliki mpya wa miamba hiyo ya Old Trafford, bilionea Sir Jim Ratcliffe na kusisitiza wamekubaliana mambo mengi.
Bilionea huyo wa Kampuni ya Ineos amenunua asilimia 25 ya hisa za klabu ya Man United na uwekezaji wake utalenga zaidi kwenye masuala ya kisoka katika timu hiyo.
Tajiri Ratcliffe alitembelea viwanja vya mazoezi ya Man United huko Carrington Jumatano iliyopita akiwa ameandamana na Mkurugenzi wa michezo, Dave Brailsford na kuwa na kikao na kocha Ten Hag.
Kocha huyo mdachi ameshuhudia matokeo mabovu ya Man United katika kipindi hiki cha msimu na kuibua wasiwasi huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea. Lakini, amepata matumaini mapya baada ya kukutana na tajiri mpya, ambaye ni shabiki mkubwa wa Man United.
“Tulikuwa na kikao kirefu, saa kibao tumeketi kuzungumza. Katika mambo mengi tulionekana kukubaliana, kila upande ulikuwa sawa. Naweza kusema kilikuwa kikao chenye kujenga, tutafanya kazi kwa pamoja.”
Kocha huyo Mdachi, Ten Hag alibainisha wamefikia uamuzi wa kuwaongezea mikataba ya miezi 12 kila mmoja wachezaji, Aaron Wan-Bissaka, Victor Lindelof na Hannibal Mejbri, huku mazungumzo ya kuhusu hatima ya mastaa Raphael Varane na Anthony Martial bado yanajadiliwa, hayajafikia mwafaka.
Tajiri mpya wa Old Trafford, Ratcliffe amepanga kuweka mezani Pauni 238 milioni, ambazo anaamini zitafaa kwenye kufanya usajili wa kuboresha kikosi ili kirudi kwenye makali yake ya zamani.
Alisema: “Nikiwa kama kijana wa hapa na shabiki wa muda mrefu wa hii klabu, nimefurahi sana kukubaliwa na Bodi ya Man United kutupa ruhusa ya kusimamia masuala ya kisoka ya klabu.
“Wakati mambo ya kibiashara yakiendelea kufanikiwa, klabu pia itahakikisha ina pesa za kutosha kwa ajili ya kushinda mataji ili kurudi kwenye makali yake, ambayo yametoweka miaka ya karibuni.
“Tutaleta maarifa ya dunia, wataalamu na vipaji ili kuboresha klabu, huku tukitoa pesa pia kwa ajili ya uwekezaji kwenye Uwanja wa Old Trafford. Tupo hapa kwa ajili ya mipango ya muda mrefu, hivyo tunafahamu changamoto nyingi mbele yetu, tutakabiliana nazo kisomi.
“Tupo hapa kufanya kazi na kila mtu, bodi, wafanyakazi, wachezaji na mashabiki ili kusaidia klabu kusonga mbele. Dhamira yetu ipo wazi, tunataka kuiona Man United ikirejea inakostahili, kuwa nafasi za juu kwenye soka la England, Ulaya na dunia.”
Man United itashuka uwanjani Jumatatu na itasafiri hadi DW Stadium kukabiliana na Wigan Athletic katika mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la FA.