Bruno Guimaraes, Manchester United kuna kitu
Muktasari:
- Mashetani Wekundu wanadaiwa kuwa katika mazungumzo ambayo yanalenga dirisha lijalo la kiangazi.
MANCHESTER United inadaiwa kwamba ipo katika mazungumzo ya mwisho ya kumsajili nahodha wa Newcastle United na timu ya taifa ya Brazil, Bruno Guimaraes, 28, kwa ada inayokadiriwa kufikia Pauni 69.
Mashetani Wekundu wanadaiwa kuwa katika mazungumzo ambayo yanalenga dirisha lijalo la kiangazi.
Hata hivyo, dili hilo linaweza kuwa gumu baada ya Real Madrid kuonyesha upya nia ya kumtaka kiungo huyo ambaye kazi yake ni kubwa uwanjani. Mbali ya Real Madrid, upande mwingine Newcastle imeonyesha msimamo wa kutotaka kumpoteza Guimaraes, na tayari imeanza mipango ya kufanya mazungumzo ya kumpa mkataba mpya unaoweza kuvunja rekodi ili kumbakisha katika kikosi.
Hali hiyo inaonekana kuwa itazidisha ugumu kwa Man United ambayo inatafuta kiungo anayeweza kuziba pengo la Casemiro aliyetangaza kuondoka mwisho wa msimu.
Mkataba wa Guimaraes unatarajiwa kumalizika ifikapo 2028 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 35 za michuano yote, amefunga mabao tisa na kutoa asisti saba.
Marcus Rashford
INAELEZWA Manchester United imekataa maombi ya Barcelona ili kumsajili kwa mkopo wa msimu mmoja zaidi mshambuliaji wa kimataifa wa England, Marcus Rashford, 28, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mashetani Wekundu wanasisitiza kuwa Barca inatakiwa kulipa ada ya Pauni 26 milioni ili kumsajili mazima Rashford ambaye msimu huu yupo katika kikosi hicho kwa mkopo. Hadi sasa bado haijaeleweka kama Barca itakubali kulipa kiasi hicho au la.
Cristian Romero
BEKI wa kimataifa wa Argentina, Cristian Romero, 27, amepuuza tetesi za kuondoka Tottenham Hotspur katika dirisha lijalo la usajili. Romero ameweka wazi kuwa kwa sasa lengo lake kubwa ni kuisaidia Tottenham kupambana na hatari ya kushuka daraja Ligi Kuu England na hajafanya uamuzi wowote juu ya hatima yake. Hivi karibuni tovuti nyingi zilidai nyota huyo ameshafanya hadi makubaliano kadhaa na timu vigogo kutoka Ligi Kuu Hispania.
Randal Kolo Muani
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ufaransa, Randal Kolo Muani, 27, anayekipiga kwa mkopo Tottenham Hotspur akitokea PSG anatajwa kuwa kwenye rada za Juventus. Inaelezwa kuwa Juventus inapanga kumsajili staa huyo ambaye amewahi kucheza katika kikosi hicho msimu uliopita.Kwa sasa Tottenham Hotspur haionyeshi nia ya kumsainisha mkataba wa moja kwa moja supastaa huyo.
Mohamed Salah
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Misri, Mohamed Salah, 33, bado hajafanya uamuzi kuhusu mustakabali wake ndani ya kikosi cha Liverpool licha ya tetesi zinazomhusisha na matajiri wa Saudi Arabia. Inaelezwa kuwa Al-Hilal ipo katika mazungumzo na wawakilishi wake na tayari imeshaanza kuzungumza na mkurugenzi wa michezo wa Liverpool, Richard Hughes. Mkataba wa Salah unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Youri Tielemans
KIUNGO wa kimataifa wa Ubelgiji, Youri Tielemans, 28, anadaiwa kuweka wazi kuwa hayupo tayari kukubali ofa yoyote ya kuondoka Aston Villa katia dirisha lijalo. Tielemans amekuwa akiwindwa na klabu kadhaa kutoka Saudi Arabia, lakini inaelezwa anajisikia furaha kubaki Villa Park na kuendelea na maisha yake ya soka England. Uamuzi huo unaonekana kuwa pigo kwa timu zilizokuwa zikimuwania.
Antonio Rudiger
REAL Madrid inafanya mazungumzo na beki wake wa kimataifa wa Ujerumani, Antonio Rudiger, 33, ili kumsainisha mkataba mpya katika dirisha lijalo. Rudiger amekuwa sehemu muhimu ya safu ya ulinzi ya Madrid kwa muda na klabu hiyo inaonekana kutaka kuendelea kunufaika na uzoefu wake. Mazungumzo hayo kwa sasa yamefikia hatua nzuri na kuna uwezekano mkubwa akasaini.
Marcus Tavernier
NEWCASTLE United imeanza mazungumzo ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Bournemouth na England, Marcus Tavernier, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Ripoti zinaeleza Newcastle imekuwa ikimfuatilia Tavernier kwa muda mrefu na inaamini anaweza akavaa vyema viatu vya Sandro Tonali ambaye haonekani kuwa na asilimia nyingi za kubaki. Mkataba wa sasa wa Tavernier unamalizika 2029.