Mourinho amtaka beki Calafiori aletwe Real Madrid
Muktasari:
- Hatua hiyo ni ya kushangaza kwa kuwa Mourinho ndiye aliyeruhusu Calafiori kuondoka AS Roma mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 1.5 milioni kwenda FC Basel. Miaka miwili baadaye, Arsenal walimsajili kwa Pauni42 milioni.
Kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho anataka kumsajili beki wa Arsenal, Riccardo Calafiori, kama sehemu ya mpango wake wa kuijenga upya timu hiyo yenye maskani yake kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Hatua hiyo ni ya kushangaza kwa kuwa Mourinho ndiye aliyeruhusu Calafiori kuondoka AS Roma mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 1.5 milioni kwenda FC Basel. Miaka miwili baadaye, Arsenal walimsajili kwa Pauni42 milioni.
Mourinho tayari ameripotiwa kufikia makubaliano ya kuwasajili Denzel Dumfries kutoka Inter Milan na Ibrahima Konate kutoka Liverpool.
Calafiori ni mchezaji muhimu Arsenal, lakini majeraha ya mara kwa mara yanaweza kuifanya Real Madrid kujaribu kuona kama inaweza kuwashawishi Arsenal kumuuza.
Bruno Fernandes
MANCHESTER United imeamua kusitisha kwa muda mazungumzo ya kuongeza mkataba wa nahodha wao, Bruno Fernandes.
Viongozi wa klabu wanaamini kiungo huyo ataendelea kubaki Old Trafford kwa muda mrefu, hivyo wameelekeza nguvu katika usajili wa wachezaji wapya.
Fernandes yupo kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake wa sasa, lakini una kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi. Inadaiwa mmiliki mwenza wa klabu, Jim Ratcliffe, ameweka kipaumbele kwenye usajili mpya.
Gabriel Jesus
EVERTON imeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Arsenal, Gabriel Jesus, dirisha hili la usajili. Hata hivyo, klabu hiyo haitaki kulipa Pauni 20 milioni zinazohitajika kwa sasa.
Everton ina wasiwasi kuhusu rekodi ya majeraha ya nyota huyo wa Brazil na inatafuta dili lenye gharama nafuu zaidi.
Vigogo wa Italia, AC Milan na Juventus, pamoja na Palmeiras ya Brazil, nao wanatajwa kufuatilia kwa karibu mustakabali wa mshambuliaji huyo.
Marco Palestra
ATALANTA inatarajia kupata angalau Euro 50 milioni iwapo watamuuza beki wao chipukizi, Marco Palestra, dirisha hili la usajili.
Nyota huyo aling’ara akiwa kwa mkopo Cagliari na hata kuitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Italia. Manchester City, Arsenal, Newcastle United na Liverpool zote zinadaiwa kuvutiwa naye. Hata hivyo, Inter Milan wanaamini wana nafasi nzuri ya kufanikisha dili hilo kwa Euro 45 milioni.
Zadok Yohanna
NEWCASTLE United wameingia kwenye mbio za kuwania saini ya winga chipukizi wa AIK, Zadok Yohanna. Nyota huyo, 18, tayari amepokea ofa kutoka Brighton & Hove Albion, huku Chelsea na Tottenham Hotspur nazo zikiendelea kufuatilia maendeleo yake.
Yohanna alijiunga na AIK akitokea akademi ya Ikon Allah ya Nigeria na amevutia kwa kiwango chake bora ndani ya muda mfupi. Ushindani wa kumpata unaendelea kuongezeka kadiri dirisha la usajili linavyokaribia kufunguliwa.
Yoane Wissa
YOANE Wissa anaweza kuondoka Newcastle United dirisha hili la usajili huku klabu hiyo ikijiandaa kufanya mabadiliko makubwa kikosini. Newcastle imeongeza uwezo wao wa kifedha baada ya kumuuza Anthony Gordon kwenda Barcelona kwa Pauni milioni 70.
Taarifa zinaeleza sehemu kubwa ya fedha hizo itatumika kuimarisha safu ya ushambuliaji. Uuzaji wa Wissa unaweza kufungua nafasi ya kusajili mshambuliaji mwingine mkubwa.
Andrea Cambiaso
BARCELONA wanaonekana kuongoza mbio za kumsajili beki wa Juventus na timu ya taifa ya Italia, Andrea Cambiaso. Nyota huyo mwenye miaka 26 aliwahi kuwa karibu kuhamia Manchester City mwaka 2025, lakini dili hilo halikufanikiwa. Chelsea pia wamehusishwa na beki huyo, lakini taarifa za hivi karibuni zinaonyesha Barcelona ndiyo wanaopewa nafasi kubwa zaidi ya kupata saini yake.
Gianluca Mancini
INTER Milan wanamfuatilia kwa karibu beki wa AS Roma, Gianluca Mancini, dirisha la usajili la kiangazi. Nyota huyo bado ana mkataba Roma hadi mwaka 2027, lakini mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya yameripotiwa kusimama kwa sasa. Mabingwa hao wa Serie A wanaamini Mancini anaweza kuwa nyongeza muhimu katika kikosi chao msimu ujao.