Bukayo Saka arejea uwanjani tayari kuivaa Madrid

Muktasari:
- Staa huyo wa The Gunners alipigwa picha kwa mara ya kwanza akiwa mazoezini huko London Colney baada ya kuwa nje ya uwanja muda mrefu tangu alipofanyiwa upasuaji wa misuli ya paja Desemba mwaka jana.
LONDON, ENGLAND: BUKAYO Saka amebakiza hatua chache sana kabla ya kuanza kuonekana tena uwanjani na uzi wake wa Arsenal.
Staa huyo wa The Gunners alipigwa picha kwa mara ya kwanza akiwa mazoezini huko London Colney baada ya kuwa nje ya uwanja muda mrefu tangu alipofanyiwa upasuaji wa misuli ya paja Desemba mwaka jana.
Na Saka aliwashtua mashabiki wake kwenye mtandao wa Instagram, alipoposti picha inayomwonyesha akiwa na tabasamu pana pamoja na kuonyesha ishara ya dole gumba na kuandika: “Habari zenu tena.”
Kinachoelezwa ni kwamba Saka anajaribu kujiweka fiti ili awepewe nafasi ya kuwakabili Fulham, Jumanne ijayo kabla ya kipute matata kabisa dhidi ya Everton na Real Madrid.
Saka, 23, alipata maumivu ya misuli ya paja kwenye mechi ya ushindi wa mabao 5-1 kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace, Desemba 21 kabla ya kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha tatizo hilo siku chache baadaye.
Kwa muda aliokuwa nje ya uwanja alikosa mechi 19 za michuano yote, kwenye kipindi ambacho timu yake ya Arsenal imejikuta ikitupwa nje ya Kombe la FA na Kombe la Ligi na kuondoka kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England. Mpango wa Arsenal ni kuhakikisha Saka anakuwa fiti kwa ajili ya mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, ambapo mchezo wa kwanza utafanyika uwanjani Emirates, Aprili 8.
Kocha Mikel Arteta amepanga kumpa Saka dakika chache za kucheza kwenye mechi za Fulham uwanjani Emirates na ile dhidi ya Everton uwanjani Goodison Park, Aprili 5.
Arsenal haitaki sana kumlazimisha Saka kucheza ili asipate matatizo mengine yatakayomrudisha kwenye benchi, hivyo wanasubiri kuona kama anakuwa fiti kwa asilimia 100 kwa ajili ya kuanza kutumika.
Kocha Arteta alisema: “Natumaini atakuwa na uwezo wa kuuchezea mpira zaidi kwenye miguu yake kuliko ilivyokuwa. Nikiwa na maana ataweza kupiga pasi, kupiga mashuti na kukokota na mengineyo.”
“Tunataka kumpatia mazoezi makali kuona kitu gani atafanya.”
Licha ya kuumia na kuwa nje ya uwanja muda mrefu, lakini Saka amekuwa sambamba na timu yake akienda kwenye mechi mbalimbali bila ya kujali kwamba anatembelea magongo. Saka alifuatana na timu yake kwenda Dubai kwenye mazingira ya joto wakati timu hiyo ilipokwenda kuweka kambi wakati ligi iliposimama.
Kwenye kambi hiyo ya Dubai ndiko ambako Arsenal ilimpoteza staa wake mwingine, Kai Havertz, ambaye naye ameumia misuli itakayomfanya kuwa nje ya uwanja hadi msimu ujao, huku straika Gabriel Jesus naye akikosekana kwa muda mrefu ndani ya uwanja hadi msimu ujao.
Hadi anaumia, Saka alikuwa amefunga mabao tisa na asisti 13 kwenye michuano yote akiwa na kikosi cha Arsenal msimu huu.