Dah! Olympique Lyon yamponza Onana

Muktasari:
- Taarifa za ndani zilizoripotiwa na tovuti ya The Sun, zinadai kwamba kuondolewa kwake kikosini kulitokana na baadhi ya wachezaji kuomba atolewe kutokana na makosa aliyofanya katika mchezo wa Europa League Alhamisi dhidi ya Olympique Lyon.
MANCHESTER, ENGLAND: KIPA wa Manchester United aliondolewa katika kikosi kilichosafiri kwenda Newcastle jana kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle United.
Taarifa za ndani zilizoripotiwa na tovuti ya The Sun, zinadai kwamba kuondolewa kwake kikosini kulitokana na baadhi ya wachezaji kuomba atolewe kutokana na makosa aliyofanya katika mchezo wa Europa League Alhamisi dhidi ya Olympique Lyon.
Hata hivyo, kocha wa Man United, Ruben Amorim amemwambia kipa huyo wa kimataifa wa Cameroon kwamba amempumzisha tu na atarudi tena langoni kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya timu hiyo ya Ufaransa Alhamisi ya wiki hii na Onana mwenyewe amekubaliana na uamuzi huo.
Licha ya ombi la wachezaji wenzake kutaka aondolewe kikosini, Amorim yeye anaamini kipa huyo alihitaji siku chache za kupumzika na kutuliza akili baada ya wiki ngumu.
Kabla ya mchezo dhidi ya Lyon, Onana aliingia katika vita ya maneno na kiungo wa zamani wa Mashetani Wekundu hao, Nemanja Matic.
Mserbia huyo adai hadharani kwamba Onana ni mmoja kati ya makipa wa ovyo zaidi kuwahi kudakia Man United katika historia ya kabu hiyo.
Baada ya kauli hiyo, Onana naye aliibuka na kusema licha ya ubovu wake bado amefanikiwa kushinda medali akiwa na timu hiyo jambo ambalo Matic hakuwahi kufanikisha.
Hata hivyo, maneno ya Matic yalionekana yana ukweli ndani yake kwani Onana alifanya makosa mawili ambayo yalisababisha mechi hiyo kumalizika kwa sare.
Hayo yalikuwa kati ya makosa mengi aliyofanya kipa huyo wa zamani wa Inter tangu afike England miaka miwili iliyopita.
Maisha ya Onana ndani ya Jiji la Manchester hivi karibuni yanaonekana kuwa na changamoto nyingi kwani mbali ya kutofanya vizuri kiwanjani, mke wake pia alikumbana na tukio la uvamizi.
Tukio hilo lilisababisha familia yake ihitaji ulinzi wa saa 24 nyumbani kwao huko Cheshire ili isijirudie tena tukio la aina hilo.
Man United inadaiwa kupanga kusajili kipa kwa msimu ujao ambapo inahusishwa na makipa mbalimbali akiwamo Joan Garcia kutoka Espanyol.