De Bruyne anaondoka Man City na mihela yake

Muktasari:
- De Bruyne anaondoka Man City akiwa ametengeneza rekodi kibao na kuacha historia ya kutosha kutokana na mchango wake alioutoa katika timu hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: TAARIFA iliyopo ni nyota wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin de Bruyne ataondoka katika kikosi hicho mwisho wa msimu huu, baada ya kukitumikia kwa takribani miaka 10.
De Bruyne anaondoka Man City akiwa ametengeneza rekodi kibao na kuacha historia ya kutosha kutokana na mchango wake alioutoa katika timu hiyo.
Hata hivyo, mbali ya rekodi na historia, staa huyu pia ametengeneza pesa za kutosha na kuwa mmoja wa wachezaji matajiri duniani.
ANAPIGAJE PESA
Utajiri wake kwa kiasi kikubwa umetokana na mshahara anaoupokea Manchester City wa Pauni 400,000 kwa wiki na kuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa pesa nyengi Ligi Kuu England. Pia ana mikataba na kampuni mbalimbali zinazomlipa pesa nyingi ikikadiriwa kufikia zaidi ya Pauni 5 milioni kwa mwaka, ikiwamo kutoka kampuni za Sure Bets, Nike, Credit Karma, Wow Hydrate, Therabody, Emirates na Electronic Arts combined. Pia ana udhamini mnono wa kampuni ya McDonald's na kwa jumla ana utajiri unaofikia Dola 70 milioni.

MJENGO
De Bruyne ana mjengo wa kifahari huko Alderley Edge, moja ya maeneo ya kifahari zaidi ya Cheshire katika Jiji la Manchester ambako kuna kundi kubwa la wachezaji kutoka Ubelgiji.
De Bruyne anamiliki jumba la ghorofa tatu na anaishi na mkewe na watoto wake watatu.
Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 32, pia anamiliki nyumba maeneo ya Bolderberg, Ubelgiji na hiyo aliijenga mwaka 2019 na ndani yake una uwanja wa mpira wa kikapu, Jacuzzi na uwanja mdogo wa soka.

MSAADA KWA JAMII
Kevin De Bruyne na mkewe Michele ni wadhamini wa Shirika la Ronald McDonald Fund for Children, shirika lisilo la kiserikali linalosaidia familia zenye watoto wanaoumwa magonjwa makubwa.
Staa huyu pia aliwahi kushiriki katika kampeni ya kusaidia mpango wa afya ya akili kwa vijana na alitoa jezi yake iliyouzwa kisha pesa zilizopatikana ndizo zilitumika kuchangia huko.

NDINGA
Rolls-Royce Ghost
Range Rover Sport
Mercedes-Benz GLE Coupe
Mercedes-Benz G63
Ferrari 488

MAISHA BINAFSI
Kevin yupo kwenye ndoa na Michele Lacroix ambaye alimchumbia mwaka 2014 kisha wakaoana Juni 2017 na tangu hapo wamepata watoto watatu.
Staa huyu sio mmoja kati wachezaji wanaopenda sana kwenda kujirusha, anapokuwa mapumzikoni hupendelea zaidi kukaa nyumbani.