De Lima tajiri asiye na makuu

SAO PAULO, BRAZIL. NANI asiyemjua, Ronaldo Luis Nazario De Lima? Labda kwa watoto waliozaliwa kuanzia mwaka 2005, kwani alistaafu soka mwaka 2011 na sasa ni mfanyabiashara mkubwa anayeingiza pesa nyingi kwa madili yake hayo.
Ni mwanasoka bora wa dunia kwa miaka miwili (Ballon d’Or mwaka 1997 na mwaka 2002) na kwa soka aliloonyesha kwa kipindi chake, tuzo kibao alizobeba na makombe kibao akiwa na klabu alizocheza na timu ya taifa Brazil, jina lake lilikua kwa kasi na kutengeneza pesa ndefu.
Sasa akiwa mfanyabiashara, anamiliki vitega uchumi ingi vinavyomfanya awe kati ya matajiri waliowahi kucheza soka na kufanya uwekezaji.
Amezichezea timu mbalimbali kama Cruzeiro alikoanzia soka lake, PSV, Barcelona, Inter Milan, Real Madrid, AC Milan na Corinthians alikostaafia soka na alitamba pia na timu ya taifa ya Brazil.
Biashara zake anazomiliki ziko nchi za Brazil na Hispania zinazomwingizia kipato cha kutosha.
ANAPIGAJE PESA
Wakati anacheza soka alisaini mkataba wa maisha na Kampuni ya Nike wenye thamani ya Dola 180 milioni na ni balozi wa Kampuni ya Pirelli, Snickers na Santander Bank na kila moja humpatia kiasi kisichopungua Pauni 10 milioni kila mwaka. Pia amewekeza kwenye biashara mbalimbali zinazomweka kwenye ramani ya wachezaji wa zamani wenye pesa nyingi.
Anamiliki hisa za asilimia 45% katika kampuni ya 9ine Sports and Entertainment agency inayosimamia wachezaji na wasanii na kufanya kazi nyingine za kimichezo na burudani nje ya uwanja.
Mara kadhaa amewahi kuonekana kwenye matangazo ya televisheni ya Pirelli commercials.
Anamiliki hisa asilimia 82 kwenye klabu ya Real Valladolid inayoshiriki Ligi Kuu Hispania na kuwa miongoni wa wamiliki wa timu hiyo na hisa nyingine anamiliki kwenye timu ya Fort Lauderdale Strikers ya Amerika.
Pia anamiliki hoteli kadhaa nchini kwao Brazil na kijumla miradi yote hiyo inamwingizia Dola 70 milioni kwa mwaka na kufanya utajiri wake kufikia Dola 300 milioni.
MIJENGO
Ana mijengo Brazil na Hispania na mara nyingi hupendelea zaidi kukaa kwenye mjengo wake uliopo Hispania alioujenga kwenye kisiwa cha maraha cha Ibiza.
Nyumba hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 10 milioni, huku nyumba yake ya Brazil inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 7 milioni.
NDINGA
Rolls Royce Cullinan
Bugatti Veyron
Lamborghini Aventador
Bugatti Centodieci
Maserati GranCabrio
Bugatti Chiron
Audi RS7
Mercedes Benz GLE63s AMG
Rolls Royce Phantom Drophead
Ferrari 599 GTO
MSAADA KWA JAMII
Aliwahi kuwa balozi wa amani wa Umoja wa mataifa, pia amekuwa akisaidia taasisi mbalimbali zinazolewa watoto yatima huko nchini Brazil.
Ameanzisha taasisi iitwayo Fundacao Fenomenos (Phenomona Foundation) inayowekeza kwenye miradi ya kusaidia jamii Brazil. Pia akademi yake iitwayo R9 Ronaldo Academy yenye matawi Marekani, China na Brazil.
BATA NA MAISHA BINAFSI
Yupo kwenye ndoa na mrembo Celina Locks wakiwa kwenye uhusiano tangu mwaka 2015, kabla ya hapo aliwahi kuoa wanawake watatu ambao ni Maria Beatriz Antony, Daniella Cicarelli na Milene Domingues aliozaa nao watoto wanne ambao ni Ronald Domingues, Maria Sophia, Alexander Nazario na Maria Alice.
Jamaa anapenda sana kuponda raha licha ya kuchapa kazi.