Droni za tiba kutumika Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Ndege hizo zitakuwa na vifaa kama defibrillator (kifaa cha kurejesha mapigo ya moyo), Epipen (sindano ya dharura kwa wagonjwa wa mzio mkali) na vifaa vya huduma ya kwanza, ambapo zitawekwa tayari katika viwanja mbalimbali Marekani, Canada na Mexico ili kusaidia kuhakikisha usalama wa kiafya.
MIAMI, MAREKANI: Viwanja vya Kombe la Dunia 2026 vitatumia ndege zisizo na rubani maarufu droni zenye vifaa vya uokoaji maisha ili kutoa msaada wa haraka wakati wa dharura za kiafya kwa mashabiki.
Ndege hizo zitakuwa na vifaa kama defibrillator (kifaa cha kurejesha mapigo ya moyo), Epipen (sindano ya dharura kwa wagonjwa wa mzio mkali) na vifaa vya huduma ya kwanza, ambapo zitawekwa tayari katika viwanja mbalimbali Marekani, Canada na Mexico ili kusaidia kuhakikisha usalama wa kiafya.
Droni hizo zina uwezo wa kufika moja kwa moja katika eneo maalumu ndani ya uwanja na pia zitakuwa na vifaa vya mawasiliano (redio). Endapo kutatokea dharura, watu waliopo karibu na mgonjwa wataweza kuwasiliana moja kwa moja na wahudumu wa afya waliopata mafunzo maalumu.
Katika miaka ya karibuni, imekuwa jambo la kawaida kuona mechi zikisitishwa kutokana na dharura za kiafya zinazowapata mashabiki jukwaani.
Kutokana na hali hiyo, matumizi ya droni yanatarajiwa kusaidia huduma kufika kwa haraka zaidi kwa wahitaji, huku pia yakipunguza usumbufu wa kusimamisha mchezo kwa muda mrefu. Kampuni ya Motorola Solutions, ambayo inahusika na masuala ya usalama katika mashindano hayo, itatumia droni za aina ya Guardian.
Droni hizo zina uwezo wa kubeba mzigo wa hadi kilo 4.5, jambo linalozifanya ziweze kupeleka vifaa muhimu katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika haraka. Mbali na vifaa vya huduma ya kwanza, droni hizo zitabeba defibrillator, Epipen na redio ili kurahisisha mawasiliano kati ya watu waliopo eneo la tukio na huduma za dharura.
Motorola Solutions pia inashirikiana na kampuni ya SkySafe katika juhudi za kuzuia droni zisizoidhinishwa kuingia katika anga la viwanja vya michezo na maeneo ya mazoezi.
Teknolojia hiyo inaweza kuvuruga mawasiliano kati ya droni isiyotakiwa na mwendeshaji wake, jambo linaloweza kuifanya ishindwe kuendelea kuruka. Hata hivyo, mbinu hiyo haitarajiwi kutumika wakati ambapo kuna umati mkubwa wa watu.
Pia kutatumika mbinu ya 'GPS spoofing' ambapo droni isiyoidhinishwa hupotoshwa kwa kupewa taarifa za eneo zisizo sahihi na kuelekezwa sehemu nyingine.
Aidha, droni maalumu za usalama zinaweza kutumia nyavu nyepesi kuzinasa droni hatari na kuzifanya zishindwe kuendelea kuruka.
Mifumo yote hiyo inaweza kutumika katika mji wa Kansas City, ambapo timu ya England inatarajiwa kufanya mazoezi yake kwa faragha bila kufuatiliwa na watu wasiohusika.