Prime
England itakavyoingiza timu saba Ligi ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:
- Arsenal inakabiliwa na shughuli pevu kwenye robo fainali ikitakiwa kuivaa Real Madrid baada ya kuitawala PSV kwenye 16 bora.
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England inaweza kutawala soka la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa kuwa na timu saba zitakazoshiriki mikikimikiki hiyo.
Uefa imefanya mabadiliko makubwa kwenye michuano hiyo msimu huu, mtindo mpya wa hatua ya makundi uliohusisha mpira wa ligi na kuwa na msimamo mmoja, kabla ya kufikia hatua ya 16 bora iliyoonyesha uhondo mkubwa wa soka kwa mashabiki. Ligi Kuu England bado ina timu zake kwenye michuano hiyo baada ya Arsenal na Aston Villa kutinga hatua ya robo fainali.
Arsenal inakabiliwa na shughuli pevu kwenye robo fainali ikitakiwa kuivaa Real Madrid baada ya kuitawala PSV kwenye 16 bora. Wakati upande wa Aston Villa ya Unai Emery itakuwa na kasheshe la kuikabili Paris Saint-Germain baada ya kupenya bila shida mbele ya Club Brugge.
Ikiwa bado kuna mambo kibao ya kusubiri na kuona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, lakini mtazamo sasa umehamia msimu ujao, kujua ni timu ngapi zitashiriki michuano hiyo kutokea England.

England ina nafasi ngapi Ligi ya Mabingwa Ulaya?
Kwa hapa ilipo, Ligi Kuu England ina nafasi nne za timu kufuzu moja kwa moja kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Timu nne zinazomaliza nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo, ndizo zinazokamatia tiketi hiyo ya kufuzu moja moja. Kwa msimamo ulivyo kwa sasa, timu hizo nne za juu ni Liverpool, Arsenal, Nottingham Forest na Chelsea. Lakini, mambo yanaweza kubadilika kutoka sasa hadi mwisho wa msimu kwa sababu hadi timu inayoshika namba 10 Fulham inaweza kufuzu kwa sababu kati yake na timu nyingine za juu kuna tofauti ya pointi saba tu. Timu kibao ikiwamo Manchester City, Newcastle, Brighton, Aston Villa na Bournemouth zote zina matumaini ya Top Four.
Nafasi ngapi za ziada?
Wakati nafasi za kufuzu moja kwa moja zikifahamika wazi, utaratibu mpya wa UEFA kuhusu tiketi ya michuano hiyo unazidi kuvuruga na kuchochea upinzani. Uefa imetoa nafasi mbili za ziada kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na hizo zitakwenda kwa chama washirika wao kulingana na pointi watakazovuna kwenye msimamo wa viwango vya soka. Na viwango hivyo kwa wanachama vitapimwa kutokana na timu za nchi husika zinavyoshiriki kwenye michuano mitatu ya Uefa: Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League na Europa Conference League. Kila klabu itavuna pointi mbili endapo inashinda na pointi moja kwenye mechi ya sare. Na baada ya hapo, pointi hizo zote zinajumlishwa na kupatikana idadi kamili ya pointi ambazo imevuna nchi wanachama katika viwanja vya Uefa. Na kwa nchi itakayokuwa na pointi nyingi, itakuwa na nafasi ya kuwa na timu ya ziada kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya nje ya zile nne zinazofuzu moja kwa moja kupitia msimamo wa ligi ya ndani.

Nchi gani sasa inaongoza viwango vya Uefa?
Kwa bahati nzuri, Ligi Kuu England kwa sasa ipo kwenye nafasi nzuri ya kupata nafasi moja ya ziada kwenye ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. England kwa sasa ina pointi 108.8 na bado ina timu tano kati ya saba zilizokuwa kwenye michuano ya Ulaya.
Inafuatia Italia yenye pointi 94.7, Hispania pointi 91.5, Ujerumani ina pointi 85.5 na bado ina klabu tatu zinazoendelea kwenye michuano hiyo. Ufaransa ina pointi za chini zaidi, 70.9 huku ikiwa imebaki na timu mbili tu zinazoendelea kwenye michuano hiyo ya Ulaya.
Nafasi nyingine ni zipi?
Ishu ya timu tano imeshapata ufafanuzi zinavyoweza kuwa, lakini kuna nafasi nyingine mbili za kupigania kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya anafuzu moja kwa moja kama bingwa mtetezi, hivyo Arsenal na Aston Villa ili kujihakikishia nafasi ya kucheza michuano hiyo kwa uhakika zaidi, zinahitaji kushinda ubingwa.
Lakini, nafasi hiyo itakuwa kama tu timu hiyo iliyonyakua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya haipo kwenye nafasi ya kufuzu moja kwa moja kupitia ligi ya ndani. Hilo lipo hivyo pia kwenye ishu ya mshindi wa Europa League kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya moja kwa moja.
Hiyo ina maana, Manchester United au Tottenham Hotspur zitakuwa na nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuiongezea nafasi England endapo kama zitashinda ubingwa wa Europa na kisha hazipo kwenye nafasi za kufuzu kupitia ligi ya ndani, kwamba hazipo kwenye Top Four.

Ina maana gani kwa michuano mingine Ulaya?
Hapo ndipo panapoleta utamu. Kama hilo likitokea, basi England inaweza kuwa na timu 11 kwenye michuano ya Ulaya msimu ujao, lakini vitu vingi vya huko juu vinapaswa kutokea kwanza.
Kwa ilivyo kawaida, timu nne za juu kwenye msimamo zinafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya jumla na kisha kuna bonasi ya Uefa kulingana na chati za ubora. Kama Aston Villa itashinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Man United au Spurs ikashinda ubingwa wa Europa League, huku washindi wao hao wote wawe wamemaliza ligi kwenye nafasi ya nane, tisa au 10, hiyo itafanya England kuwa na nafasi nyingine mbili za ziada kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hiyo ina maana, tiketi ya kucheza Europa League itashuka hadi kwenye timu zitakazoshika nafasi ya 6 na 7 kwenye msimamo, huku mshindi wa Kombe la FA, hiyo haijalishi kama mshindi wa Kombe la FA awe amemaliza kwenye nafasi saba za juu. Chelsea naye inaweza kufuzu kucheza Europa League endapo kama itashinda ubingwa wa Conference League na kisha ikamaliza nafasi ya nane, tisa au 10 kwenye msimamo wa ligi.
Hilo litafanya Ligi Kuu England timu yake moja itakayokuwa kwenye Conference League ni ile itakayokuwa imemaliza ligi nafasi ya 11. Na kwa kuutazama msimamo ulivyo kwa sasa, timu hiyo ni Crystal Palace.