FIFA yakoleza utamu usajili wa mastaa EPL

Muktasari:
- Utaratibu wa usajili kwenye Ligi Kuu England kwa dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu linaweza kuwa na wiki 12, wakati lile la majira ya baridi, ambalo ni la Januari litakuwa la mwezi mmoja.
LONDON, ENGLAND: MAMBO ni moto. Ligi Kuu England inaweza kuwa na madirisha mawili ya usajili wa majira ya kiangazi mwaka huu baada ya klabu kupiga kura na kukubaliana jambo ya hilo.
Utaratibu wa usajili kwenye Ligi Kuu England kwa dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu linaweza kuwa na wiki 12, wakati lile la majira ya baridi, ambalo ni la Januari litakuwa la mwezi mmoja.
Lakini, kuwapo kwa usajili wa muda wa Fifa ambao umepangwa mwaka huu kwa ajili ya kuzipa timu zinazoshiriki Kombe la Dunia la Klabu kufanya usajili mapema umebadilisha kanuni zote.
Mikataba ya wachezaji kwa kawaida inafika ukomo Juni 30, mwisho wa msimu na kwamba wachezaji wanaweza kujiunga na klabu mpya kuanzia Julai 1. Lakini, Fifa imetangaza kwamba klabu 32 zitakazoshiriki kwenye Kombe la Dunia la klabu zinaruhusiwa kusajili wachezaji wapya kati ya Juni 1 na Juni 10.
Na kwa kuwa Chelsea na Manchester City ambazo ni timu pekee za Ligi Kuu England zitakazoshiriki michuano hiyo yenye thamani ya Pauni 770 milioni itakayofanyika Marekani, watakuwa na ruhusa ya kufanya usajili mapema.
Na taarifa ya EPL ilisomeka hivi: “Klabu za Ligi Kuu England zimekubaliana juu ya tarehe ya ya usajili wa majira ya kiangazi 2025. Dirisha litafunguliwa mapema, kati ya Jumapili, Juni 1 na Jumanne, Juni 10, kutokana na kalenda ya Fifa kwa ajili ya Kombe la Dunia la Klabu. Baada ya hapo litafungwa na kufunguliwa tena, Jumatatu, Juni 16 na kufungwa Jumatatu, Septemba mosi.”
Ligi Kuu England inajaribu kuweka dirisha lake la usajili kwenda sawa na ligi nyingine za Ulaya ili kujiepusha na hatari ya kufunga mapema wakati wengine wakiendelea kusajili jambo litakalowaweka kwenye wakati mgumu wa kutafuta wabadala endepo kama wachezaji wao watanaswa na timu za kutoka kwenye ligi nyingine.