Hatma ya Sancho, Chelsea iko hivi

Muktasari:
- Chelsea walirejea mchezoni baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili na kupata sare ya 2-2 dhidi ya Ipswich Town walioko hatarini kushuka daraja.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca alitoa taarifa kuhusu mustakabali wa Jadon Sancho baada ya mchezaji huyo kufunga bao la kusawazisha kwa Chelsea dhidi ya Ipswich Town.
Chelsea walirejea mchezoni baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili na kupata sare ya 2-2 dhidi ya Ipswich Town walioko hatarini kushuka daraja.
Baada ya mchezo huo wa kuvutia uliopigwa kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, Kocha Maresca alitoa taarifa kuhusu hatma ya winga huyo wa kimataifa wa England.
Sancho alijiunga na Chelsea kwa mkopo kutoka Manchester United majira ya joto yaliyopita na mkataba wake ulikuwa na kipengele cha kumnuna kwa lazima ikiwa Chelsea watamaliza kwenye nafasi 14 za juu katika Ligi Kuu England.
Kipengele hicho kinaitaka Chelsea kutoa ada ya uhamisho kati ya Pauni 22 hadi 24 milioni itategemea na nafasi ambayo itamaliza.
Hata hivyo, kumekuwa na ripoti pia zinazodai, Chelsea haina mpango wa kumsainisha mkataba wa kudumu na badala yake watalipa Pauni 5 milioni kama fidia ya kutofanya hivyo kwa staa huyo ambaye hakuanza katika mechi iliyopita.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari baada ya mechi yao dhidi ya Ipswich, Maresca ambaye ni raia wa Italia alisema:
“Aanafanya vizuri. Leo tuliamua kuanza na Pedro na Noni. Noni amerudi kutoka kwenye majeraha, alifunga mara mbili kabla ya hapa, Pedro naye anafanya vizuri. Na Jadon anacheza karibu kila mechi.”
“Mpango ulikuwa tu kumpumzisha kidogo, kuhusu mustakabali wake, kwa kweli sasa ndiyo wakati wa kufikiria lakini bado tuna mwezi mmoja umebakia, kwanza acha tumalize msimu vyema na baada ya hapo tutafanya maamuzi.”