Italia yasikilizia ofa ya mezani Kombe la Dunia
Muktasari:
- Italia ilipoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-1 dhidi ya Bosnia inayonolewa na Edin Dzeko, na ikashindwa kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo, jambo linalochukuliwa kama anguko kubwa katika historia ya soka la taifa hilo.
MILAN, ITALIA: TIMU ya taifa ya Italia ina matumaini madogo ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia, mwaka huu, licha ya kutolewa kwa aibu na Bosnia katika mechi ya mchujo ya kuwania kufuzu, ambapo kwa sasa italazimika kusikilizia ofa ya upendeleo.
Italia ilipoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-1 dhidi ya Bosnia inayonolewa na Edin Dzeko, na ikashindwa kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo, jambo linalochukuliwa kama anguko kubwa katika historia ya soka la taifa hilo.
Hata hivyo, kuna uwezekano mdogo sana wa wao kushiriki mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, ikiwa Iran itashindwa kwenda. Kumekuwa na sintofahamu kubwa kuhusu ushiriki wa Iran kutokana na mvutano wa kisiasa na Marekani, ambaye ni mmoja wa waandaaji wa mashindano hayo.
Marekani na Israel walifanya shambulio la makombora dhidi ya Iran, Februari, mwaka huu, lililosababisha kifo cha kiongozi wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei.
Kutokana na hali hiyo, waziri wa michezo wa Iran amesema nchi yao “haina uwezekano wa kushiriki” mashindano hayo, huku rais wa Marekani Donald Trump akipendekeza Iran ijiondoe kwa “usalama wao wenyewe.”
Trump aliandika: “Timu ya taifa ya Iran inakaribishwa Kombe la Dunia, lakini sidhani ni sahihi kushiriki kwa sababu ya usalama wao.”
Kwa sasa, hakuna uamuzi rasmi uliotolewa. Kwa mujibu wa kanuni za FIFA, chombo hicho kina mamlaka ya mwisho kuamua nini kifanyike ikiwa Iran itajiondoa.
Hali hiyo inadaiwa kuwa inaweza kuipa Italia nafasi ya kushiriki, hasa kwa kuwa ni moja ya timu zilizo na viwango vya juu kati ya zile ambazo hazijafuzu.
Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa zaidi kuwa FIFA itachukua timu nyingine kutoka Asia ili kudumisha uwiano wa idadi ya timu kutoka kila shirikisho.