Kane mambo safi, arudi mazoezini

Muktasari:
- Staa huyo wa Bayern Munich ameonekana kwenye mazoezi ya klabu yake akijaribu kujiweka sawa kurejea uwanjani baada ya kusumbuliwa na majeraha.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA, Harry Kane anapiga hatua nzuri katika kupona maumivu ya misuli yanayomkabili ambayo awali yalitishia uwezekano wa kuwa nje kwa muda mrefu.
Staa huyo wa Bayern Munich ameonekana kwenye mazoezi ya klabu yake akijaribu kujiweka sawa kurejea uwanjani baada ya kusumbuliwa na majeraha.
Nahodha huyo wa England alipata majeraha ya maumivu ya paja lake la kulia katika mchezo wa sare ya bao 1-1 baina ya Bayern na Borussia Dortmund mwezi uliopita na awali ilidhaniwa asingeonekana tena uwanjani mwaka huu hadi 2025.
Hata hivyo, Kocha wa Bayern, Vincent Kompany amefichua amepata matumaini makubwa Kane anaweza kurejea uwanjani kabla ya Bundesliga haijasimama kukwepa kipindi cha baridi. Kompany anaamini Kane atakuwa fiti kucheza mchezo wa mwisho wa Bundesliga kabla ya kusimama kupisha kipindi cha baridi dhidi ya RB Leipzig, Ijumaa.
“Anafanya vizuri. Amekuwa akifanya mazoezini. Matumaini atakuwa fiti kwa ajili ya mechi ijayo,” alisema Kompany baada ya mechi ya kichapo cha mabao 2-1 ilichopata Bayern Munich kutoka kwa Mainz na kuongeza: “Harry Kane na Alphonso Davies waliweza kufanya mazoezi Jumatatu kwa mara ya kwanza.”
Kane alipata maumivu ya misuli katika mechi dhidi ya Dortmund, wakati Davies alipata maumivu kama hayo katika mechi dhiid ya Heidenheim.
Tatizo la majeruhi linaonekana kuiandamana Bayern kutokana na kipa wao Manuel Neuer naye kuwa nje ya uwanja.
Badaa ya kukumbana na kichapo cha kwanza kwenye Bundesliga msimu huu dhidi ya Mainz, Jumamosi, jambo hilo limefanya waongoze ligi kwa tofauti ya pointi moja tu dhidi ya Bayer Leverkusen.
Kane amefunga mabao 14 na kuasisti mara tano katika mechi 12 alizocheza kwenye Bundesliga msimu huu.