Kikao kizito... Rashford, Amorim kuyamaliza kikubwa

Muktasari:
- Kikao hicho pia kinadaiwa kuwa na lengo la kuweka mambo sawa kati yao kabla ya timu kusafiri kwenda Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim atafanya mazungumzo na mshambuliaji wa timu hiyo, Marcus Rashford mwisho wa msimu kujua hatma yake ikiwa atarudishwa kikosini au ataondoka jumla.
Kikao hicho pia kinadaiwa kuwa na lengo la kuweka mambo sawa kati yao kabla ya timu kusafiri kwenda Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu.
Rashford kwa sasa yuko kwa mkopo Aston Villa, baada ya kutokea kwa mvutano kati yake na kocha Amorim uliosababisha aondolewe kikosini kisha kutolewa kwa mkopo Januari mwaka huu.
Mkataba wake wa mkopo na Villa unamalizika mwishoni mwa mwezi Juni, wiki chache kabla ya Man United kusafiri kwenda Marekani kujiandaa kwa msimu mpya. Villa wana nafasi ya kumnunua Rashford moja kwa moja kwa Pauni 40 milioni ikiwa watataka kufanya hivyo, lakini hadi sasa bado hawajafanya uamuzi.
Iwapo Villa hawatamnunua, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England atarejea Man United ingawa hatma yake bado haijulikani.
Man United wako tayari kumuuza Rashford, lakini kama hakuna klabu itakayomchukua kufikia mwisho wa mwezi wa Julai, atajumuishwa kwenye kikosi kitakachoingia kambini kwa maandalizi ya msimu mpya.
Mabosi wa juu wa Man United wanataka Rashford na Amorim kumaliza tofauti zao ili fundi huyu arudi kikosini na kuendelea kuitumikia timu.
Amorim alisema Rashford hakuwa anajituma mazoezini ikiwa ni siku kadhaa tu baada ya staa huyo kufanya mahojiano na kusema anataka kuondoka kwani hapati nafasi ya kutosha. Amorim amekataa kuzungumzia suala la Rashford katika wiki za hivi karibuni, akisisitiza kuwa anajikita tu kwa wachezaji alio nao kikosini.