King Salah ni rekodi baada ya rekodi England

Muktasari:
- Winga huyo alimaliza uvumi kuhusu mustakabali wake katika kikosi cha Liverpool, Ijumaa ya wiki iliyopita kwa kusaini mkataba mpya wa miaka miwili unaomwezesha kupata Pauni 380,000 kwa wiki.
LIVERPOOL, ENGLAND: IKIWA ni siku chache tangu asaini mkataba mpya, mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah amewekea rekodi nyingine katika Ligi Kuu England.
Winga huyo alimaliza uvumi kuhusu mustakabali wake katika kikosi cha Liverpool, Ijumaa ya wiki iliyopita kwa kusaini mkataba mpya wa miaka miwili unaomwezesha kupata Pauni 380,000 kwa wiki.
Mkataba wa awali wa Salah ulitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na ilidaiwa kwamba huenda angeondoka.
Salah amevunja rekodi ya kuhusika katika mabao mengi na pasi za mabao kwenye msimu mmoja ambapo kiujumla amehusika katika mabao 45.
Salah sasa amempiku Thierry Henry, aliyekuwa anashikilia rekodi hiyo aliyoiweka msimu wa 2002/03 na alihusika katika mabao 44 pamoja na straika wa Manchester City, Erling Haaland, alihusika katika mabao sawa na hayo.
Baada ya rekodi hiyo, Salah anatarajiwa kuweka rekodi nyinginr inayomkodolea macho ambayo inashikiliwa na Alan Shearer na Andrew Cole, waliohusika katika mabao 47 wakati huo ligi ikiwa na mechi 42. Shearer aliweka rekodi akiwa na Newcastle wakati Cole akiwa na Blackburn.
Salah amekuwa katika kiwango bora sana msimu huu ambapo amefunga mabao 27 na kutoa asisti 18.
Kabla ya kusaini mkataba mpya, Salah alikuwa akihusishwa na kuhamia Saudi Arabia na Novemba mwaka huu aliweka wazi yupo karibu kuondoka kuliko kubakia.
“Bila shaka nina furaha sana. Tuna timu nzuri sasa kama ilivyokuwa zamani, nimesaini mkataba mpya wa sababu naamini tuna nafasi kubwa ya kshinda makombe na nitakuwa na wakati mzuri,” alisema Salah baada ya kusaini mkataba mpya.