Kuhusu Cunha, Amorim kasema haweki neno

Muktasari:
- Amorim alikuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari na alisisitiza itakuwa ngumu kwake kutabiri ikiwa staa huyo atajiunga na timu au laa.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amekataa kutoa maoni kuhusu tetesi zinazoihusisha timu hiyo na nyota wa Wolves, Matheus Cunha, anayedaiwa anaweza kusajiliwa dirisha lijalo.
Amorim alikuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari na alisisitiza itakuwa ngumu kwake kutabiri ikiwa staa huyo atajiunga na timu au laa.
Nyota huyo wa Brazil anayetakiwa na timu nyingi kubwa barani Ulaya ana kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu hiyo inayomhitaji italipa Pauni 62.5 milioni na Man United iko tayari kulipa kiasi hicho.
Inaaminika Cunha ‘ana matumaini’ uhamisho wake kwenda Old Trafford utakamilika mwisho wa msimu huu, licha ya timu nyingine kama Chelsea na Arsenal kuonyesha nia ya kumsajili.
“Sitosema chochote kuhusu Matheus, kwa sababu nikisema mara moja, nitakuwa nalazimika kusema kila wakati kama ni ndiyo au hapana. Hivyo sitatoa maoni yoyote. Ni vigumu kutabiri nini kitatokea siku za usoni.”
Ripoti nyingine zinaeleza, uwezekano wa staa huyo kutua Man United utategemea na kushinda kwao taji la Europa League ambako wapo hatua ya nusu fainali.
Kwa sasa Man United ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, na baada ya kupoteza dhidi ya Wolves – timu anayochezea Cunha wiki chache zilizopita, matumaini ya Man United yamebaki kweny Europa League pekee.