Maguire atolewa kwa Inter, yenyewe inamtaka Solet
Muktasari:
- Taarifa kutoka Italia zinaeleza, Maguire ambaye ni nyota huyo wa England ametolewa kwa mabingwa hao wa Serie A kupitia mawakala wake, huku klabu hiyo ikiendelea kutathmini chaguo mbalimbali za kuimarisha safu ya ulinzi.
Beki wa Manchester United, Harry Maguire, ameibuka katika rada za Inter Milan dirisha la usajili la majira ya kiangazi, ingawa pia kipaumbele kikubwa kwa miamba hiyo ya Italia ni Oumar Solet kutoka Udinese.
Taarifa kutoka Italia zinaeleza, Maguire ambaye ni nyota huyo wa England ametolewa kwa mabingwa hao wa Serie A kupitia mawakala wake, huku klabu hiyo ikiendelea kutathmini chaguo mbalimbali za kuimarisha safu ya ulinzi.
Inter wanatarajia kufanya mabadiliko makubwa kikosini baada ya baadhi ya mabeki wao wenye uzoefu kuwa mbioni kuondoka.
Francesco Acerbi na Matteo Darmian wanatarajiwa kuondoka mwishoni mwa mikataba yao, huku mustakabali wa Stefan de Vrij ukiendelea kuwa wa mashaka.
Aidha, Yann Bisseck anahusishwa na kuhamia Bayern Munich, jambo linaloweza kuacha pengo kubwa zaidi katika safu ya ulinzi.
Hata hivyo, Maguire bado si kipaumbele cha kwanza kwa Inter kwa sasa na Nerazzurri wameelekeza nguvu zao katika harakati za kumsajili Solet kabla ya kuangalia chaguo nyingine.
Maguire, 33, bado ana mkataba Manchester United hadi mwaka 2027, lakini uwezekano wa kuondoka Old Trafford unaendelea kupewa nafasi kubwa.
Bradley Barcola
Mustakabali wa mshambuliaji wa PSG, Bradley Barcola, unaendelea kuzua mjadala mkubwa Ulaya. Liverpool na Arsenal zimeonyesha nia ya kumsajili, lakini endapo atapatikana sokoni, klabu nyingi kubwa zinatarajiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro.
Winga huyo wa Ufaransa anathaminiwa kwa kasi na ubunifu wake, jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa wanaotazamwa kwa karibu.
Alisson Becker
Liverpool wanatarajia kipa wao Alisson Becker kubaki Anfield licha ya Juventus kuonyesha nia ya kumsajili. Alisson amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, lakini kuna kipengele cha kuongeza kwa miezi 12 zaidi.
Klabu hiyo inamwona kuwa sehemu muhimu ya mipango yao ya muda mrefu na haina haraka ya kuachana naye katika dirisha hili.
Yves Bissouma
Kiungo wa Tottenham Hotspur, Yves Bissouma anatarajiwa kuondoka kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu huu.
Tayari klabu ya Galatasaray ya Uturuki imeonyesha nia ya kumsajili. Mustakabali wa kiungo huyo wa Mali unaendelea kuwa wa mashaka huku akitafutwa na timu kadhaa zinazotaka kuimarisha safu ya kiungo.
Elliot Anderson
Manchester City inaongoza katika mbio za kumsajili kiungo Elliot Anderson wa Nottingham Forest, licha ya kuvutiwa pia na Manchester United na Arsenal.
Forest wanadaiwa kutaka zaidi ya pauni milioni 100 kwa kiungo huyo chipukizi. Anderson ameendelea kuonyesha kiwango bora msimu huu, hali inayoongeza ushindani kati ya vigogo hao wa Ligi Kuu England wanaotaka huduma yake.
Carlos Baleba
Manchester United bado wanamfuatilia kiungo Carlos Baleba wa Brighton & Hove Albion. Thamani yake ya Pauni milioni 100 ilizuia uhamisho wake msimu uliopita na Januari, lakini United wanatarajia bei hiyo inaweza kushuka.
Klabu hiyo inaamini kiungo huyo wa Cameroon anaweza kuwa sehemu muhimu ya maboresho ya kikosi msimu ujao iwapo makubaliano yatafikiwa baina yao.
Morgan Rogers
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amewataka wamiliki wa klabu hiyo kuonyesha dhamira katika dirisha la usajili la majira ya joto baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu England na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ameweka wazi kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolengwa ni Morgan Rogers wa Aston Villa. Arteta anataka “uamuzi muhimu” ili kuipeleka Arsenal kiwango kingine, huku Rogers akiwa miongoni mwa malengo makuu ya usajili wa kiangazi.
Julian Alvarez
Arsenal na FC Barcelona ni miongoni mwa klabu kubwa za Ulaya zinazomfuatilia mshambuliaji wa Atlético Madrid, Julián Álvarez. Hata hivyo, Atletico hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo wa Argentina, ambaye bado ana miaka minne kwenye mkataba wake.
Klabu hiyo inamthamini kwa zaidi ya pauni milioni 130, jambo linalofanya uhamisho wake kuwa mgumu katika dirisha hili la usajili licha ya mvuto mkubwa kutoka Ulaya.