Mo Salah aitisha kikao cha dharura
Muktasari:
- Ikiwa Salah ataamua kubaki, itakuwa habari kubwa kwa Liverpool kutokana na mchango wake mkubwa kwa klabu hiyo tangu alipojiunga mwaka 2017, ambapo amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika historia ya kisasa ya timu hiyo.
Mshambualiji Mohamed Salah anaweza kubadili uamuzi wa kuondoka Liverpool baada ya kutimuliwa kwa Arne Slot. Salah na Slot waliripotiwa kuwa na tofauti za mara kwa mara msimu huu.
Liverpool imechukua uamuzi wa kumfuta kazi Slot baada ya kufanya tathmini ya mwisho wa msimu.
Kwa mujibu wa kundi la wanahabari watano wenye ushawishi mkubwa kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Salah ameitisha kikao cha dharura na wakala wake kujadili kuondoka kwa Slot na uwezekano wa kubadili msimamo wake kuhusu kuondoka Liverpool.
Ripoti hiyo pia ilidai: “Mohamed Salah yuko tayari kurejea Liverpool ikiwa klabu itamfikia. Hii imekuja mara tu baada ya habari za kushtua za kutimuliwa kwa Arne Slot.”
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba taarifa hizi bado zinabaki kuwa uvumi wa soko la usajili na hakuna tamko rasmi kutoka kwa Salah au Liverpool lililothibitisha kuwa amebadilisha rasmi uamuzi wake.
Ikiwa Salah ataamua kubaki, itakuwa habari kubwa kwa Liverpool kutokana na mchango wake mkubwa kwa klabu hiyo tangu alipojiunga mwaka 2017, ambapo amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika historia ya kisasa ya timu hiyo.
Marcus Rashford
Mustakabali wa mshambuliaji Marcus Rashford unaendelea kuwa gumzo kubwa barani Ulaya. Mshambuliaji huyo wa England alijiunga na Barcelona kwa mkopo akitokea Manchester United, huku mkataba wake wa mkopo ukitarajiwa kumalizika Juni 30.
Hata hivyo, uvumi kuhusu uwezekano wa Jose Mourinho kujiunga na Real Madrid na kumjumuisha Rashford katika mradi wake mpya umezua maswali mengi kuhusu hatua yake inayofuata.
Katika akaunti yake rasmi ya Instagram, Rashford alichapisha picha pamoja na video ya baadhi ya matukio yake bora akiwa na jezi ya Barcelona. Kilichovutia zaidi mashabiki na wachambuzi wengi ni maneno aliyoyaandika kwenye maelezo ya chapisho hilo. Akiambatanisha picha hizo, Rashford alieleza furaha yake akiwa Barcelona na kuashiria kuwa bado anatamani kupata mafanikio zaidi akiwa klabuni hapo.
Xabi Alonso
Xabi Alonso tayari ameanza kushawishi mipango ya usajili wa Chelsea kabla hata ya kuanza rasmi kazi yake Stamford Bridge. Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka minne kuanzia Julai 1, na inaelezwa kuwa tayari anashiriki katika mipango ya usajili.
Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa sana ni Arda Guler, ambaye inadaiwa bado anaendelea kuwasiliana binafsi na Alonso.
Nicolas Jackson
Nicolas Jackson anatarajiwa kurejea Chelsea baada ya kipindi chake cha mkopo katika Bayern Munich.
Vyanzo vya ndani ya klabu vinaeleza kuwa mshambuliaji huyo bado anathaminiwa na viongozi wa Chelsea.
Inaelezwa kuwa sababu kuu ya kuondoka kwake kwa mkopo ilikuwa ni uhusiano mbaya na kocha wa zamani Enzo Maresca.
Kwa kuwa Maresca hayupo tena, kuna uwezekano Jackson akabaki na kufanya kazi chini ya Alonso. Hata hivyo, mustakabali wake bado haujaamuliwa kwani klabu kadhaa za England na nje ya nchi zimeonyesha nia ya kumsajili.
Rafael Leao
Manchester United imeweka jina la Rafael Leao katika orodha ya wachezaji wanaowindwa kwa ajili ya kuimarisha safu ya ushambuliaji. Nyota huyo wa AC Milan anatarajiwa kupatikana kwa bei nafuu baada ya Milan kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Hata hivyo, vyanzo vinaeleza kuwa Leão siyo lengo kuu la Manchester United kwa sasa, licha ya kuvutia vilabu kadhaa vikubwa barani Ulaya.
Tijjani Reijnders
Atletico Madrid imeonyesha nia ya kumsajili kiungo Tijjani Reijnders kutoka Manchester City. Mholanzi huyo alijiunga na City mwaka mmoja uliopita akitokea AC Milan kwa pauni milioni 46.5 na alicheza mechi 47 huku akifunga mabao saba na kusaidia timu kushinda mataji mawili.
Lakini kutokana na nafasi yake kutokuwa ya uhakika katika sehemu ya pili ya msimu, Atlético inachunguza uwezekano wa kumpata.
Jean-Matteo Bahoya
Mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt, Jean-Matteo Bahoya, amekuwa akivutia klabu nyingi kutoka England na sehemu nyingine za Ulaya.Pia, klabu vya Saudi Arabia zimeonyesha nia kwa nyota huyo. Al Hilal ilijaribu kumsajili mwezi Januari, huku Al Ittihad nayo ikionyesha nia msimu uliopita.
Bahoya, ambaye ni mchezaji wa timu ya vijana ya Ufaransa chini ya miaka 21, anashikilia rekodi ya mchezaji aliyewahi kukimbia kwa kasi kubwa zaidi katika historia ya Bundesliga.
Vagiannidis
Everton imefufua nia yake ya kumsajili beki wa kulia wa Sporting CP, Georgios Vagiannidis. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ureno, ada ya euro 10 milioni inaweza kutosha kukamilisha usajili huo. Kiasi hicho ni kidogo kuliko euro12.5 milioni pamoja na nyongeza ambazo Sporting ililipa kwa Panathinaikos ili kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Ugiriki msimu uliopita. Everton ilikuwa ikimfuatilia Vagiannidis kabla hajajiunga na Sporting lakini ilishindwa katika mbio za kumpata wakati huo.