Arne Slot aondoka Liverpool
Muktasari:
- Mabingwa wa msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu England, walifanikiwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Brentford katika mchezo wa mwisho wa msimu ambao pia nyota wa kikosi hicho, Mohamed Salah aliondoka rasmi.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imemfuta kazi kocha Arne Slot, huku Andoni Iraola aliyeachana na Bournemouth mwishoni mwa msimu ulioisha akitajwa kuongoza miongoni mwa wanaotajwa kwenda kuchukua nafasi yake.
Mabingwa wa msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu England, walifanikiwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Brentford katika mchezo wa mwisho wa msimu ambao pia nyota wa kikosi hicho, Mohamed Salah aliondoka rasmi.
Slot mwenye umri wa miaka 47, aliiongoza Liverpool kutwaa Ligi Kuu England baada ya kumrithi Jurgen Klopp, lakini kulitetea kwa kiwango kibovu na kumaliza nafasi ya tano kumesababisha viongozi wenye ushawishi ndani ya klabu kuamua kuchukua mwelekeo tofauti.
Taarifa ya klabu hiyo ilisema: “Huu ulikuwa uamuzi mgumu kwetu kama klabu, na ni jambo lisilo na shaka. Mchango ambao Arne ametoa kwa Liverpool FC katika kipindi chake hapa umekuwa mkubwa, wenye maana na muhimu zaidi kwa mashabiki na kwetu. Kwa pamoja tumefikia hitimisho kwamba mabadiliko ni muhimu ili klabu iendelee kusonga mbele.
“Tunamtakia kila la heri Arne katika hatua inayofuata ya kazi yake ya ukocha, huku tukiamini kwamba ataendelea kuwa na mafanikio. Tunafanya hivyo tukijua kwamba urithi wake Liverpool bado upo na utaendelea kuwa na maana zaidi katika miaka na miongo ijayo. Hata hivyo, hitimisho tulilofikia limejengwa juu ya imani kwamba mwelekeo wa timu unaweza kushughulikiwa vyema zaidi kupitia mabadiliko ya dira..."
Hatua hiyo imekuja wiki chache tu baada ya Mohamed Salah kutoa kauli kali iliyomlenga Slot, ambapo Mmisri huyo alikosoa mtindo wa uchezaji wa Liverpool kupitia ujumbe wa kushangaza kwenye mitandao ya kijamii.
Alisema: “Nimeishuhudia klabu hii ikitoka kwa wanaotiliwa shaka hadi kuwa waumini, na kutoka kwa waumini hadi kuwa mabingwa. Kuporomoka kwetu hadi kufungwa tena msimu huu kulikuwa jambo la kuumiza sana na si kile ambacho mashabiki wetu wanastahili. Nataka kuona Liverpool ikirejea kuwa timu ya mashambulizi makali ambayo wapinzani wanaogopa na kurejea kuwa timu inayoshinda mataji..."
Slot aliiongoza Liverpool kushinda mechi 66 katika kipindi cha mechi 113 alizokinoa kikosi hicho cha Merseyside.