Haaland afurahishwa na memes zake
Muktasari:
- Badala ya kulalamikia hali hiyo, mshambuliaji huyo raia wa Norway, amekuwa akiichukulia kama sehemu ya umaarufu wake, huku wakati mwingine akishiriki baadhi ya memes hizo kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
WAKATI wachezaji wengi wakikerwa wanapogeuzwa kituko kwenye mitandao ya kijamii (meme), mshambuliaji wa Manchester City na timu ya taifa ya Norway, Erling Haaland amesema anafurahishwa na hali hiyo kufuatia vituko vinavyotengenezwa kumuhusu yeye kwani ni sehemu ya burudani yake nje ya soka.
Akizungumza kupitia chaneli yake ya YouTube, Haaland amesema baadhi ya picha na video zinazotengenezwa na mashabiki wake humfanya acheke, huku akiwataka watu kutokuwa wakali sana kwa kwenye mambo ya kuburudisha.
"Memes zimekuwa kali mno, ni balaa kabisa. Unatakiwa tu ucheke nazo, watu siku hizi wanachukulia mambo mengi kwa uzito sana," amesema mshambuliaji huyo.
Nyota huyo wa Norway, amesema hajawahi kuona sababu ya kukasirishwa na utani unaofanywa na mashabiki, ili mradi tu haukiuki mipaka yake, akiamini soka linapaswa pia kuwa chanzo cha burudani nje ya dakika 90 za uwanjani.
Katika mazungumzo hayo, Haaland alichekesha zaidi aliporejea moja ya memes zilizozua gumzo wakati wa Kombe la Dunia 2026, ambapo mashabiki walimlinganisha na kitunguu kutokana na nywele zake ndefu za rangi ya dhahabu.
"Angalia, hata kitunguu kinafanana na mimi. Ni sawa kabisa," amesema huku akicheka.
Wakati wa Kombe la Dunia 2026, Haaland alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotawala mitandao ya kijamii, huku picha na video mbalimbali zikimtania kwa kumlinganisha na wahusika wa katuni, wapiganaji wa Viking na hata vitu vya kawaida vya nyumbani.
Badala ya kulalamikia hali hiyo, mshambuliaji huyo raia wa Norway, amekuwa akiichukulia kama sehemu ya umaarufu wake, huku wakati mwingine akishiriki baadhi ya memes hizo kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, nyota huyo amewakumbusha mashabiki kuwa si kila video inayosambaa mtandaoni ni ya kweli, akieleza kuwa baadhi ya klipu zinazomuonyesha kwenye matukio ya kuchekesha zimetengenezwa kwa teknolojia ya akili bandia (AI) au face swap.
Pamoja na hilo, Haaland amesema ataendelea kufurahia utani unaowafanya watu watabasamu, akiamini kuwa kucheka ni sehemu ya maisha kama ilivyo kufunga mabao uwanjani.