Mdomo wa Raphinha umeiponza Brazil

Muktasari:
- Kwenye mechi hiyo, Brazil ilikubali kichapo cha mabao 4-1, ambapo Argentina ilitembeleza kipigo hicho kwa mabao ya Julian Alvarez, Enzo Fernandez, Alexis Mac Allister na Giuliano Simeone.
BUENOS AIRES, ARGENTINA: MASTAA wa Argentina wamesema kauli ya staa wa Kibrazili Raphinha ndiyo iliyowapa hasira na kuhakikisha wanaishushia kipigo kizito Brazil kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 kwa upande wa Amerika Kusini.
Kwenye mechi hiyo, Brazil ilikubali kichapo cha mabao 4-1, ambapo Argentina ilitembeleza kipigo hicho kwa mabao ya Julian Alvarez, Enzo Fernandez, Alexis Mac Allister na Giuliano Simeone.
Na hilo liliifanya Argentina kuwa timu ya kwanza ya Amerika Kusini kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2026.
Sare ya Uruguay kwa Bolivia kwenye mechi ya mapema iliyofanyika Jumanne kulitoa nafasi kwa mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia kukamatia tiketi yao ya fainali hizo zitakazopigwa Marekani, Canada na Mexico, lakini waliamua kuifanyia udhalilishaji mkubwa Brazil katika mechi iliyofanyika Buenos Aires.
Fowadi wa Wolves, Matheus Cunha alifungia Brazil bao hilo la kujifariji baada ya makosa ya beki wa kati wa Argentina, anayekipiga kwenye kikosi cha Tottenham, Cristian Romero. Katika mechi hiyo, Raphinha, ambaye aliongea sana kabla ya mechi, aliishia kugongesha mwamba tu kwa mpira wake wa friikiki.
Mwaka 2023, Argentina ilizifikisha mwisho rekodi ya Brazil ya kucheza nyumbani muda mrefu bila ya kupoteza, kitu ambacho Raphinha alidai kwamba kwenye mechi hiyo ya Jumanne wanakwenda Argentina kuwapiga.
Akizungumza na gwiji wa Brazil, Romario, staa huyo wa Barcelona alisema hivi: “Tunakwenda kuwapiga ndani na nje ya uwanja ikihitajika. Nitawafunga.” Kisha Raphinha aliwaambia wenzake: “Twende Argentina, tukagonge kikwelikweli.”
Kocha wa Argentina, Lionel Scaloni alijaribu kuipoza kauli hiyo ya Raphinha wakati alipojibu, alipoelezea timu hizo kwamba wanakuwa vitani uwanjani, lakini ni marafiki wakubwa nje ya uwanja.
Wakati mchezo huo unaelekea mwisho, mashabiki wa Argentina walikuwa wakiimbia nyimbo kwamba Raphinha atolewe.
Licha ya kutokuwa na huduma ya Lionel Messi na Lautaro Martinez, mastaa wa Argentina walipania mechi hiyo ili kumkomesha Raphinha na kauli yake.
Scaloni alisema: “Namwombea msamaha kwa sababu hakufanya vile kwa kupenda. Alikuwa akijaribu kuitetea nchi yake, nina hakika hakutaka kumkasirisha yeyote. Brazil itabaki kuwa Brazil, wapo kwenye kipindi kigumu, lakini watarudi.”
Alvarez alisema: “Unajua hupaswi kuongea mapema kama yale kwenye mechi kama hizi.” Na kiungo, Leandro Paredes aliongeza: “Huwezi kusema vitu kama vile halafu huwezi kufanya kitu uwanjani.”
Brazil sasa inakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Ecuador Juni, kisha itakipiga na Paraguay, timu nyingine ngumu.