Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya ni ‘fainali kabla ya fainali'

UEFA Pict

Muktasari:

  • Arsenal ndiyo pekee kutoka Ligi Kuu England iliyosalia katika michuano hiyo na vigogo wenzake Liverpool, Chelsea na Manchester City zenye mashabiki wengi zikiaga mapema.

LONDON, ENGLAND: BAADA ya vigogo wakubwa wa soka Ulaya kuaga mashindano katika hatua ya roibo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, minong'ono imebaki kwa nne zilizofuzu nusu fainali, nani atatinga fainali? Haitabiriki.

Arsenal ndiyo pekee kutoka Ligi Kuu England iliyosalia katika michuano hiyo na vigogo wenzake Liverpool, Chelsea na Manchester City zenye mashabiki wengi zikiaga mapema.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya Hispania, miamba Barcelona na Real Madrid zimetupowa nje na ndizo zilizokuwa zikiangaliwa kama zitafika nusu ama fainali ya michuano hiyo. Hata hivyo zilikumbana na vichapo kutoka kwa Atletico Madrid na Bayern Munich mtawalia na safari yao kuishia robo fainali..

Nusu fainali itazikutanisha Arsenal dhidi ya Atletico Madrid, huku Bayern ikikipiga na Paris Saint-Germain na macho na masikio yatakuwa kwa Arsenal ambayo inasaka taji lake la kwanza la michuano hiyo mikubwa Ulaya.

Arsenal iliibuka na ushindi wa jumla wa bao 1-0 dhidi ya Sporting, huku   Bayern Munich ikiichapa Real Madrid jumla ya mabao 6-4, PSG ikaichapa Liverpool 4-0 na Atletico Madrid iliiondosha Barcelona kwa mabao 3-2.

Katika hatua ya nusu fainali, mechi za mkondo wa kwanza zinatarajiwa kuanza kupigwa kati ya Mei 05 na 06 na ya kwanza itakuwa ni kati ya Arsenal itakayokuwa nyumbani kuikaribisha Atletico Madrid Saa 4:00 usiku.

Vilevile, mechi nyingine ya mkondo wa kwanza ya hatua hiyo itakuwa ni kati ya  Bayern itayokuwa nyumbani kumkaribisha bingwa mtetezi, PSG, Mei 06 kuanzia Saa 4:00 usiku.

Hadi sasa, rekodi zinaonyesha Arsenal na Atletico zimekutana katika mechi tatu za michuano ya kimataifa, moja ikiwa ni Ligi ya Mabingwa Ulaya na mbili za Europa League.

Katika mechi hizo, hakukuwa na mbabe kwani Arsenal ilishinda mara moja ambayo ilikuwa ni katika ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku mechi mbili za Europa moja ilimalizika kwa sare na nyingine Atletico ikaibuka na ushindi. Mara ya mwisho kwa miamba hii kukutana ilikuwa mwaka 2018, tangu Arsenal ikiwa chini ya Arsene Wenger.

Katika mechi hii ya Arsenal na Atletico vita kubwa inaonekana kuwa katika maeneo mawili. Atletico imekuwa ikitumia washambuliaji wawili katika michuano hii.

Kwanza ni Julian Alvarez ambaye ndio mchezaji wao hatari zaidi akiwa ndio anaongoza kwa mabao katika Ligi ya Mabingwa katika kikosi chao hadi sasa akiwa ameingia kambani mara sita.

Alvarez pia amekuwa akicheza sambamba na Antoine Griezmann ambaye katika mechi mbili zilizomalizika zote hakumaliza.

Changamoto kubwa kwa Arsenal inaonekana huenda ikawa katika safu yao ya ulinzi na William Saliba na Gabriel Magalhaes, watakuwa na shughuli ya kuwazuia Griezmann na Alvarez.

Muda mwingi, Griezmann ndio huonekana akikaa katikati ya mabeki wawili wakati, hali inayompa Alvarez nafasi kubwa zaidi ya kucheza na kufunga.

BARCA (1)

Arsenal ina pigo kubwa la kukosa baadhi ya wachezaji wao muhimu ambao wanauguza majeraha, ikiwemo Noni Madueke ambaye aliumia katika mechi iliyopiga dhidi ya Sporting Lisbon.

Vilevile inauguza majeraha ya Bukayo Saka, Martin Odegaard, Jurrien Timber na Riccardo Calafiori ambao wote hawakuwepo katika mechi dhidi ya Sporting Lisbon.

Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa wanaonekana kuwa wataisumbua zaidi Atletico katika eneo la katikati ya kiwanja ambapo Martin Zubimendi na Declan Rice wamekuwa wakitawala eneo hilo katika mechi nyingi.

Atletico mara kadhaa hupendelea zaidi kuruhusu wapinzani wao wacheze kisha wao kufanya mashambulizi ya kushtukiza kupitia Marcos Llorente, Koke ambao mara nyingi wamekuwa wakihusika katika kupokonya mipira kisha kuisogeza kwa Giuliano Simeone na Ademola Lookman ambao husogeza mashambulizi kwa kasi kwenda eneo la mwisho ambako huwakuta Alvarez na Griezmann.

Mechi ya PSG na Bayern inaonekana kuwa ndio itakuwa na utamu zaidi kutokana na ubora wa timu zote mbili na kile ambacho zimeonyesha katika mechi za robo fainali.

Kwanza timu hizi zimekutana mara 15 katika michuano hii, na mara zote hizo hakuna mechi iliyomalizika kwa sare. PSG imeshinda mechi sita huku Bayern ikishinda tisa.

MATOKEO Pict

Bayern ambayo imefuzu kwa kuichapa Real Madrid, jumla ya mabao 6-4, moja kati ya nguvu yao kubwa ni eneo lao la ushambuliaji ambapo kwa sasa Harry Kane ndio anashika nafasi yapili katika orodha ya wafungaji bora wa michuano hiyo.

Kwa kiasi kikubwa Bayern imekuwa ikitumia maeneo ya pembeni kupandisha mashambulizi ambako huwatumia Michael Olise na Alphonso Davies katika kufanikisha hilo.

Mastaa hawa hupiga krosi au pasi mbele ya mdomo wa goli na kuwapa nafasi mastaa wengine wa safu ya ushambuliaji hususani Kane kuweza kupiga na kufunga. Mara kadhaa pia Olise amekuwa akipiga mwenyewe akitokea upande wa kulia, huku Davies yeye mara nyingi akionekana kupiga pasi zaidi badala ya kufunga.

Kuelekea mechi yao dhidi ya PSG sehemu inayoonekana nyasi zitang'oka sana ni ile ya pembeni ambako kuna Achraf Hakimi upande wa kulia na Nuno Mendes upande wa kushoto katika safu ya ulinzi.

Ubora wa PSG kwa kiasi kikubwa unaonekana kwenye safu yao ya kiungo inayoongozwa na fundi Vitinha akiwa pamoja na Joao Neves na Zaire Emery ambao wamekuwa wakimlisha sana Ousmane Dembele ambaye timu nzima inaonekana kucheza nyuma yake.

Hii inaweza kuzua vita mpya kati yake na mabeki tegemeo wa Bayern, Dayot Upamecano na Jonathan Tah ambao watakuwa na shughuli ya kupambana na wachezaji watu kwa wakati mmoja.

Kwanza kabisa ni Khvicha Kvaratskhelia upande wa winga ya kushoto na Desire Doue upande wa kulia ambao nao huwa wanafanya mikimbio ya kuingia ndani ya boksi na muda mwingine hucheza katikati ya mabeki wa pembeni na wale wa kati hivyo, humpa Dembele nafasi nzuri ya kushambulia kwa sababu mabeki wa kati wa hulazimika kusogea kidogo kuwakaba Kvaratskhelia na Doue jambo linalosababisha waache nafasi kwa Dembele.