Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pep apishana na Gundogan

Muktasari:

  • Gundogan ambaye alifanya mahojiano baada ya timu yao kupata kipigo cha saba katika mechi 10 za mwisho, alisema Man City ilikuwa inacheza vibaya sana kiasi cha kupoteza mipira kirahisi na kuruhusu mabao hayo mawili  kupitia mashambulizi ya kushtukiza.

MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola alionekana kutokubaliana na tathmini ya kiungo wake Ilkay Gundogan kuhusu kichapo cha 2-0 kilichowakumba juzi, kutoka kwa Juventus katika Ligi ya Mabingwa.

Gundogan ambaye alifanya mahojiano baada ya timu yao kupata kipigo cha saba katika mechi 10 za mwisho, alisema Man City ilikuwa inacheza vibaya sana kiasi cha kupoteza mipira kirahisi na kuruhusu mabao hayo mawili  kupitia mashambulizi ya kushtukiza.

Hata hivyo, Guardiola alionekana kushangazwa alipojulishwa kuhusu maoni ya Gundogan alipokuwa akifanya mahojiano ya tovuti ya TNT Sports baada ya mechi.

“Ni jambo la kuvunja moyo sana. Tulikuwa na nafasi za kufunga mabao kadhaa lakini kwa sasa inaonekana kila shambulizi tunaloruhusu ni hatari sana. Nahisi wakati mwingine tunakuwa wazembe kidogo kwenye mapambano ya ana kwa ana, badala ya kucheza kwa urahisi tunajaribu kufanya mambo kuwa magumu zaidi, na tukakosa muda sahihi wa kuachia mpira.

“Tunapoteza mpira na kuwapa nafasi ya mashambulizi ya kushtukiza. Timu yetu imejengwa kucheza kwa  kumiliki mpira, kuuficha na kuwa imara na tunatakiwa kama huwezi kufanya lolote tusiupoteze. Kwa sasa mambo hayaendi vizuri kwetu.”

Kocha wa City alipojulishwa kuhusu maoni ya Gundogan alijibu: “Hapana, hapana, leo tumefanya vizuri labda siku nyingine lakini leo tumefanya vizuri sana. Hatukupoteza mipira mingi kama ilivyotokea zamani, tulijaribu kufika katika nafasi bora. Timu za Kiitaliano zinajua kukaba na wachezaji wanacheza karibu karibu wanajua sana kujilinda. Tulicheza kwa staili yetu, tulikosa matokeo lakini kiwango kilikuwa bora .”

Matokeo hayo yameifanya Man City kwa kiasi kikubwa kupoteza nafasi ya kumaliza kati ya timu nane bora kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa ili kufuzu moja kwa moja katika hatua ya 16-Bora, hivyo inaweza kuwalazimu kuingia hatua hiyo kwa kucheza mechi ya mtoano.

Mabingwa hawa watetezi wa EPL kwa sasa wapo nafasi ya 20, na mchezo ujao watacheza dhidi ya Paris Saint-Germain ugenini Januari mwakani kabla ya kuikaribisha Club Brugge Etihad.

Tangu mwanzo wa Novemba, Man City imeruhusu mabao 21, mengi kuliko timu yoyote ligi tano bora Ulaya.