Petit ataka washambuliaji Arsenal wauzwe
Muktasari:
- Arsenal, wikiendi iliyopita ilipoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya mchezo huo kumaliza dakika tisini kwa sare ya bao 1-1, sasa inatarajiwa kufanya maboresho kwenye kikosi chake baada ya kocha Mikel Arteta kuitaka bodi ya klabu hiyo kuwa na “matamanio makubwa zaidi†katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Petit, ameishauri klabu hiyo kuwauza Gabriel Martinelli, Noni Madueke na Gabriel Jesus kabla ya kuanza kwa msimu ujao.
Arsenal, wikiendi iliyopita ilipoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya mchezo huo kumaliza dakika tisini kwa sare ya bao 1-1, sasa inatarajiwa kufanya maboresho kwenye kikosi chake baada ya kocha Mikel Arteta kuitaka bodi ya klabu hiyo kuwa na matamanio makubwa zaidi katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
The Gunners walitwaa taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada ya miaka 22 msimu huu, lakini walikosa nafasi ya kutengeneza historia kwa kutwaa mataji mawili baada ya Eberechi Eze na Gabriel Magalhães kukosa penalti zao mjini Budapest.
Arteta anataka kuhakikisha timu yake inaendelea kupata mafanikio siku zijazo na anafahamu anahitaji maboresho upande wa kushoto wa safu yake ya ushambuliaji, pamoja na mshambuliaji wa kati, beki wa kulia na kuongeza ushindani zaidi katika eneo la kiungo.
Ili nafasi zipatikane kwa wachezaji wapya, Arsenal italazimika kuwaacha baadhi ya wachezaji wake wa sasa, huku Petit akitaka washambuliaji hao watatu waondoke.
Wakati Bukayo Saka akiwa amejihakikishia nafasi ya kudumu upande wa kulia eneo la ushambuliaji, Arsenal imekuwa ikihangaika kupata mbadala sahihi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, huku usajili wa majira ya kiangazi yaliyopita, Noni Madueke, akishindwa kuwa na kiwango cha kudumu katika nafasi hiyo.
Vivyo hivyo, upande wa kushoto wa ushambuliaji umekuwa eneo lenye changamoto kwa Arteta, ambapo Leandro Trossard na Gabriel Martinelli wamekuwa wakionyesha kiwango kisichoridhisha .
Petit aliiambia talkSPORT katika kipindi cha White and Jordan: “Nadhani ni rahisi kuona Arsenal inakosa nini; kwangu mimi ni mawinga.
“Unahitaji kuwa na mawinga wenye nguvu, kasi na uwezo mkubwa wa kiufundi ambao wanaweza kuleta tofauti pembeni mwa uwanja.”
Mshambuliaji Viktor Gyokeres, mwenye umri wa miaka 28, hajafikia kiwango kilichotarajiwa kutoka kwake wala kile alichoonyesha alipokuwa Sporting Lisbon, licha ya kufunga mabao 21 tangu aliposajiliwa kwa pauni 63.5 milioni majira ya kiangazi yaliyopita.
Kati ya mabao yake 14 ya Ligi Kuu England msimu huu, sita yalifungwa dhidi ya timu zilizopanda daraja, huku akiwa hajafunga dhidi ya timu yoyote kubwa isipokuwa mabao mawili dhidi ya Tottenham mwezi Februari.
“Kwangu mimi, wachezaji kama Martinelli na Jesus hawajafanya kazi yao ipasavyo kwa Gyokeres sijui labda ni kwa sababu ndiyo kwanza amejiunga na klabu,†alisema Petit.
“Trossard ningembakiza. Madueke kwangu hana kiwango cha kutosha. Samahani kusema hivyo, lakini anatakiwa kufanya mengi zaidi ili kuimarika. Lakini kwa hakika tunahitaji mawinga, na pengine mshambuliaji mwenye kasi, uwezo wa kiufundi na harakati bora uwanjani badala ya kupoteza mipira mingi. Tunahitaji kuboresha safu yetu ya ushambuliaji.”
Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwa kwenye rada ya Arsenal ni Morgan Rogers wa Aston Villa anayekadiriwa kuwa na thamani ya pauni 80 milioni, pamoja na mshambuliaji kijana mwenye kipaji wa Bournemouth, Eli Junior Kroupi.
Rogers amefunga mabao 10 katika mashindano yote msimu huu na anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha kocha Thomas Tuchel kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Kwa upande wake, Kroupi amefunga mabao 13 msimu huu, idadi kubwa zaidi kuwahi kufungwa na kijana wa umri wa chini ya miaka 20 katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu England, akivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Robbie Fowler na Robbie Keane. Mabao hayo yanajumuisha yale aliyofunga dhidi ya Arsenal, Manchester City na Manchester United, jambo lililomfanya kuwa kijana wa kwanza kufunga dhidi ya timu zote tatu zilizomaliza katika nafasi tatu za juu ndani ya msimu mmoja.
Trossard, ambaye alicheza mechi 31 za Ligi Kuu England msimu huu, alifunga mabao sita, huku Madueke akifunga matatu pekee katika mechi zake 26 za ligi. Gabriel Jesus naye alifunga mabao matatu tu ya ligi msimu huu. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester City amekuwa akisumbuliwa na majeraha katika kipindi chake cha miaka minne klabuni hapo, akicheza mechi 84 za Ligi Kuu England pekee kati ya 152 zilizotakiwa.