Robo fainali Euro 2024 ni kivumbi

Muktasari:
- Jambo hilo ni habari mbaya kwa England, ambayo kama itashinda dhidi ya Uswisi kwenye robo fainali itakuwa na kibarua cha kumenyana na moja ya timu hizo mbili kwenye hatua ya nusu fainali.
MUNICH, UJERUMANI: NDO hivyo. Mechi zote za hatua ya robo fainali kwenye Euro 2024 zimeshathibitishwa baada ya Uholanzi na Uturuki kuwa timu za mwisho kukamatia tiketi ya kucheza hatua hiyo ya nane bora baada ya kushinda mechi zao usiku wa juzi Jumanne.
Jambo hilo ni habari mbaya kwa England, ambayo kama itashinda dhidi ya Uswisi kwenye robo fainali itakuwa na kibarua cha kumenyana na moja ya timu hizo mbili kwenye hatua ya nusu fainali.
Uholanzi ya kocha Ronald Koeman imekamatia tiketi ya robo fainali baada ya ushindi mnono kabisa wa mabao 3-0 dhidi ya Romania.
Cody Gakpo alifunga bao la kuongoza, kabla ya mtokea benchini Donyell Malen kuja kufunga mara mbili kuifanya Oranje kusonga mbele.
Uturuki yenyewe iliichapa Austria 2-1. Merih Demiral aliifungia Uturuki bao la kuongoza kwenye dakika ya kwanza tu, kabla ya kuongeza jingine kwenye dakika 59, yakiwa mabao yake ya kwanza kwenye soka la kimataifa tangu 2022 - huku Austria bao lao alifunga Michael Gregoritsch. England ilitinga robo fainali kwa mbinde, ikihitaji bao la dakika za mwisho kabisa kupitia kwa Jude Bellingham kusawazisha mbele ya Slovakia, kabla ya kufunga la pili kwenye dakika 30 za nyongeza kwa kichwa cha Harry Kane.
Ureno ilikuwa na shughuli pevu mbele ya Slovenia, ambapo ilihitaji ushindi wa penalti 3-0 kutinga robo fainali baada ya sare ya bila kufungana kwenye dakika 120, huku Ufaransa, Hispania na Uswisi zenyewe zilimaliza kazi ndani ya dakika 90. Na sasa timu zote nane zilizofika hatua hiyo ya obo fainali zimeshafahamika, huku England ikitambua ugumu wa njia yake ya kuelekea fainali ulivyo.
England kwanza itakabiliana na Uswisi Jumamosi na kama itashinda hapo, basi itacheza na mshindi wa mechi ya Uholanzi na Uturuki kwenye nsu fainali siku nne baadaye ili kutinga fainali, itakayopigwa Berlin, Julai 14.
Kwa upande mwingine, wenyeji Ujerumani itakipiga na Hispania kwenye robo fainali baada ya hapo, mshindi atakwenda kukabiliana na mshindi kati ya Ureno na Ufaransa kwenye hatua ya nusu fainali ili kuwania tiketi ya fainali. Mechi za robo fainali zitaanza kupigwa kesho Ijumaa, wakati zile za nusu fainali zimepangwa kufanyika Julai 9.