Ronaldo afunguka kutua Man City

Muktasari:
- Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa tuzo ya za Ballon d’Or aliwahi kuwa karibu kujiunga na mabingwa hao watetezi wa EPL mwaka 2021 kabla ya dili kupinduka katika dakika za mwisho na kutua Manchester United.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo amezungumzia uwezekano wa kujiunga na Manchester City inayoonekana kuwa katika hali mbaya kwa sasa na kusisitiza kwamba timu hiyo itarudi tu katika kiwango chake.
Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa tuzo ya za Ballon d’Or aliwahi kuwa karibu kujiunga na mabingwa hao watetezi wa EPL mwaka 2021 kabla ya dili kupinduka katika dakika za mwisho na kutua Manchester United.
Hata hivyo, sasa ameonekana kufungua tena mlango wa kurejea England na kutua kwa wababe hao kutokana na kauli alizosema katika hafla ya Tuzo za Globe Soccer huko Dubai.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 39 alifichua kuwa yuko tayari kutoa “msaada” kwa Man City katika kipindi hiki kigumu wanachopatia.
Nyota huyo wa Ureno alisema: “Huwezi kujua nini kitatokea,” baada ya kauli hii mtangazaji alimuuliza amemaanisha nini, na Ronaldo akasema: “Hiyo ina maana sijakataa,” kisha akacheka.
Matumaini ya Man City kushinda taji la Ligi Kuu England kwa mara ya tano msimu huu yanaonekana kupotea kabisa kutokana na kiwango ilichoonyesha.
Vijana hawa wa Pep Guardiola wamepoteza mechi tisa kati ya 13 za michuano yote kabla ya mchezo wao dhidi ya Leicester jana ambapo walikuwa na tofauti ya pointi 14 pia na vinara Liverpool.
Hadi kufikia wikiendi iliyopita, Man City kwa sasa wako katika nafasi ya saba katika msimamo wa EPL, pointi sita nyuma ya Nottingham Forest iliyoko nafasi ya nne.
“Kila timu huwa na nyakati, kuna nyakati ngumu na nzuri, Man City wanapitia kipindi kigumu lakini nina asilimia 100 watarejea. Nadhani timu kubwa, wachezaji wakubwa ni werevu vya kutosha kuelewa shida iko wapi na tatizo liko wapi. Nina uhakika wa asilimia 100 watarejea. Guardiola ni kocha mzoefu sana. Anajua tatizo lipo wapi, muda mfupi ujao watakuwa sawa.”