Ronaldo, Toney wana bato lao

Muktasari:
- Toney, mshambuliaji wa zamani wa Brentford ya England amekuwa moto baada ya kufunga mabao 19 huku Ronaldo akiwa nayo 23.
RIYADH, SAUDI ARABIA: WAKATI timu ya Cristiano Ronaldo, Al Nassr ikitarajiwa kuukosa tena ubingwa wa Ligi Kuu Saudi Arabia (SPL), gwiji huyo anakumbana na ushindani mwingine katika kuwania kiatu cha mfungaji bora msimu huu kutoka kwa Ivan Toney anayeichezea Al-Ahli.
Toney, mshambuliaji wa zamani wa Brentford ya England amekuwa moto baada ya kufunga mabao 19 huku Ronaldo akiwa nayo 23.
Al Nassr ya Ronaldo ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Al Qadsiah juzi Ijumaa katika mechi ya ligi ikishindwa kutumia kikamilifu nafasi ya Al Ittihad ya Karim Benzema iliyoteleza mbele ya Al Fateh.
Tofauti ya pointi kati ya Al Nassr na vinara Al Ittihad inasalia kuwa pointi nane, huku zikiwa zimesalia mechi sita kumalizika kwa msimu.
Mbali na pengo hilo, Ronaldo sasa anakabiliwa na ushindani mkali katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu, kwani ushindi mkubwa wa mabao 5-0 dhidi ya Al Fayha ilioupata Al Ahli, ambapo Toney alifunga mabao mawili umeongeza presha kwake.
Toney alifunga bao kwa kichwa kabla ya lile la pili kwa penalti baada ya Riyad Mahrez, nyota wa zamani wa Manchester City kukwatuliwa ndani ya eneo la hatari. Mahrez pia alifunga bao na kumaliza aibu kwa Al Fayha, ambao sasa wako alama nne kutoka eneo la kushuka daraja. Kwa sasa Toney yupo sawa na Abderrazzaq Hamed-Allah wa Al Shabab kwenye nafasi ya pili ya wafungaji, huku Benzema akiwa na mabao 17.
Iwapo mchezaji yeyote kati yao atamzidi Ronaldo kwa ufungaji itakuwa ni pigo kubwa kwa mkongwe huyo, kwani mchezaji huyo bora wa dunia mara tano alitawala ligi hiyo tangu alipojiunga nayo Januari 2023 akitokea Man United.