Slot aiba mavitu ya Klopp Anfield

Muktasari:

  • Slot amefunguka katika wiki zake za kwanza tangu atue klabuni hapo amekuwa akitazama video mbalimbali za mazoezi na mechi za nyuma za timu hiyo ili kuiba baadhi ya vitu kutoka kwa mtangulizi wake Jurgen Klopp.

NI hivi. Ili kuendana na mambo mbalimbali ya Liverpool msimu ujao, moja ya mambo anayofanya Kocha mpya wa kikosi hicho cha Anfield, Arne Slot ni kutazama video mbalimbali zikiwamo za mazoezini na mechi za timu hiyo.

Slot amefunguka katika wiki zake za kwanza tangu atue klabuni hapo amekuwa akitazama video mbalimbali za mazoezi na mechi za nyuma za timu hiyo ili kuiba baadhi ya vitu kutoka kwa mtangulizi wake Jurgen Klopp.

Slot alisaini mkataba wa miaka mitatu wa kukinoa kikosi cha Majogoo hao akitokea Feynoord alikobeba taji la Ligi Kuu ya Uholanzi na Dutch Cup.

Alisema ni kweli anachukua baadhi ya vitu lakini litakapokuja suala la uwanjani ni lazima aingize mbinu na ufundi wake.

"Naanagalia mazoezi ili niwajue vizuri wachezaji kwa sababu wengi huwa nawaona kwenye mechi, ukitazama mazoezi unakuwa unafahamu vizuri utamaduni wa timu na wachezaji wanavyofanya mazoezini na namna walivyozoea kufanya."

"Nafikiri ni jambo zuri kuchukua mikoba ya Klopp na kujifunza baadhi ya vitu, kila kocha huwa anaiba baadhi ya vitu kwa mwenzake, mara nyingi huwa tunafanya hivyo pale tunapotazama mechi na mazoezi, kwangu mimi ni jambo zuri kwa sababu inakusaidia ujue unaanza wapi."

"Lazima kutakuwa na mabadiliko, navaa jezi mpya hivyo lazima niingize vitu vipya ingawa mambo mengi yatabaki kama hapo awali kwa sababu wachezaji ni wale wale, tutafanya kazi kwa kuanzia Klopp alipoachia, ingawa na mimi nitaingiza baadhi ya vitu vyangu kwa sababu nafahamu hilo ndilo mashabiki na watu wengi wanatarajia kuliona kutoka kwangu."