Takwimu zaibeba Barca El Clasico

Muktasari:
- Barcelona na Madrid zinakutana katika mchezo wa fainali ya Copa del Rey itakayopigwa kwenye dimba la Estadio de La Cartuja, mjini Sevilla, huku rekodi za msimu huu zikiibeba Barcelona.
SEVILLE, HISPANIA: NI wikiendi nyingine nchini Hispania, kila shabiki wa soka leo anajiandaa kushuhudia mchezo wa mkubwa zaidi wa kihistoria, Wahispania wanauita El Classico.
Barcelona na Madrid zinakutana katika mchezo wa fainali ya Copa del Rey itakayopigwa kwenye dimba la Estadio de La Cartuja, mjini Sevilla, huku rekodi za msimu huu zikiibeba Barcelona.
Barca imeinyanyasa sana Madrid timu hizo zilipokutana msimu huu ikiifunga mabao 5-2 na kutwaa SuperCup de Espana na ikaichakaza pia kwa mabao 4-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa LaLiga.
Hata hivyo, rekodi za ujumla Real Madrid imeshinda mechi nyingi zaidi ilipokutana na Barca katika michuano yote. Madrid imeshinda mechi 105, Barca imeshinda mara 102, huku mechi 52 zikimalizika kwa sare.
Licha ya ukubwa wa mechi yenyewe unaotokana na kuikutanisha miamba hii, pia ni mechi muhimu kwa timu zote kwa sababu ni nafasi ya kunyakua kikombe kwa msimu huu.
Madrid iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga, ikiwa na tofauti ya pointi nne na Barcelona, inahitaji sana kushinda taji hili kwa sababu haina uhakika wa kuchukua Ligi Kuu ambako wako nyuma, pia imeshaondolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Vilevile, kwa upande wa kocha Carlo Ancelotti anayehusishwa kuwa ataondoka mwisho wa msimu huu, kushinda taji hili kwake itakuwa sehemu ya kuondoka kwa heshima kwenye timu hiyo aliyohudumu tangu mwaka 2021.
Barcelona ambayo kwa sasa inashikilia nafasi kwanza katika La Liga, kuchukua ubingwa huu itaweka hai matumaini yake ya kushinda mataji matatu (treble) msimu huu.
Tayari Barca ipo kwenye hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambako itacheza dhidi ya Inter Milan, hivyo inaweza kushinda taji hilo na La Liga.
Katika historia, Barcelona ndio inaongoza zaidi kwa kushinda taji hili la Mfalme ikifanya hivyo mara 31 kati ya fainali 42 ilizocheza, wakati Madrid ikiwa inashika nafasi ya tatu kwa kushinda mara nyingi ikifanya hivyo mara 20 katika fainali 40.
Madrid ndio inaongoza pia katika orodha ya timu ambazo imepoteza fainali za michuano hii mara nyingi (20).