TOTAL FUTBOL: Tatu zinahitajika Ulaya 2025/26

Muktasari:
- Manchester City ni kati ya zile zinazopewa nafasi ya kushinda taji lakini kikwazo chao kikubwa kimeonekana ni mashtaka 115 ambayo yakithibitika hata watakapokuwa wamemaliza ndani ya nafasi tano za juu watajikuta wameshushwa daraja wakibainika wana makosa.
LONDON, ENGLAND: WAKATI Ligi Kuu England ikiwa inaelekea ukingoni huku ubingwa ukionekana unaenda Liverpool na nafasi ya pili ikitarajiwa kwenda kwa Arsenal, swali kubwa limekuwa ni timu gani itakayomaliza katika nafasi ya tatu hadi tano ambazo zitafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa? Kwenye nafasi hizo tatu, kuna jumla ya timu tano ambazo zinaziwania na hapa kuna uchambuzi wa timu gani zinaweza kumaliza katika nafasi hizo.
Manchester City ni kati ya zile zinazopewa nafasi ya kushinda taji lakini kikwazo chao kikubwa kimeonekana ni mashtaka 115 ambayo yakithibitika hata watakapokuwa wamemaliza ndani ya nafasi tano za juu watajikuta wameshushwa daraja wakibainika wana makosa.
Man City ambayo ina pointi 61 ikiwa katika nafasi ya tatu, itatakiwa kuendelea kupata matokeo katika michezo yake minne iliyosalia ili kumaliza katika nafasi hiyo ambapo kuna tofauti ya pointi moja tu kati yao na Nottingham iliyopo nafasi ya nne.
Mechi tano za leo Jumamosi ni ile inayoanza mapema kabisa saa 8.30 mchana ikizikutanisha Chelsea iliyo katika nafasi ya sita kwa pointi 57 dhidi ya Everton iliyo katika nafasi ya 13 na pointi zake 38 ikiwa imejihakikishia kubaki Ligi Kuu.
Kisha zitapigwa mechi nne za saa 11:00 ambazo ni kati ya Wolves itakayocheza na Leicester ambayo inapigania kutoshuka daraja, Brighton itaivaa West Ham, wakati Southampton ambayo imeshashuka daraja itacheza na Fulham, huku Wolves itaikabili Leicester City ambayo pia imeshashuka daraja.
Nottingham Forest ambayo ni moja kati ya timu zilizofanya maajabu kutokana na kiwango ilichoonyesha msimu huu chini ya Nuno Espirito Santo inaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kumaliza ndani ya nafasi tano za juu kwa msimu huu.
Forest ambayo pia ipo nusu fainali ya FA ikitarajiwa kucheza na Manchester City wikiendi hii, mechi yao ya kuamua hatima ya kumaliza ndani ya nafasi tano za juu inaonekana itakuwa ni dhidi ya Chelsea Mei 25 wote wakiwa wanagombania nafasi hiyo.
Baada ya kufanikiwa kuchukua Kombe la Carabao mbele ya Liverpool, huu ni mtihani mwingine wa Eddie Howe ambao akiufaulu atakuwa ameweka rekodi nyingine ya kuwawezesha Newcastle kufuzu michuano hiyo ya Ulaya tangu msimu wa 2022–23.
Hata hivyo, mtihani huu anaweza kuufaulu ikiwa tu, atachanga vizuri karata zake katika mechi tatu za mwisho zinazoonekana kuwa ngumu ambazo ni dhidi ya Arsenal, Chelsea na Everton.
Kwa sasa Newcastle iko nafasi ya 5 ikiwa na pointi 59.
Chelsea iko nafasi ya sita ikiwa na tofauti ya pointi mbili dhidi ya Newcastle na katika mechi zilizosalia itakuwa inaiombea mabaya Newcastle kupoteza mchezo mmoja tu, ili wao waweze kupanda ingawa itatakiwa ihakikishe inapata ushindi katika mechi zake zilizosalia.
Mtihani mzito upo katika mechi zao mbili za mwisho ambazo zitaikutanisha na wapinzani wao wa Top 5 Newcastle na Nottingham Forest.
Timu ya mwisho katika vita hii inaonekana kuwa ni Aston Villa ingawa kupoteza kwao dhidi ya Manchester City wikiendi iliyopita kwa mabao 2-1 inaonekana kuwa sababu mojawapo itakayowagharimu kutoshinda vita na kumaliza nafasi tajwa.
Sasa wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kushinda mechi zao za nyumbani dhidi ya Fulham na Tottenham, ambazo hawana rekodi nzuri kwani imeshaporeza mara 18 dhidi ya Spurs.
Nafasi ya Emery kumaliza ndani ya Top 5 inaweza ikategemea safari yao ya mwisho kwenda Old Trafford ambako pia hawana rekodi nzuri kwani katika mechi 23 za ligi zilizopita kwenye uwanja huo, Villa imepoteza mara 19, sare mbili na kushinda mara mbili.