Udambwidambwi wa Ligi Kuu England 2022-23

LONDON, ENGLAND. KESI imekwisha. Tiketi ya kuiwakilisha Ligi Kuu England kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao imeshapata wenyewe, ambapo Manchester City itaungana na Arsenal, Manchester United na Newcastle United kwenye michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu huko Ulaya.
Pazia la Ligi Kuu England likienda kufungwa kesho, Jumapili - Man City ndio walionyakua taji hilo, wakifanya hivyo kwa msimu wa tatu mfululizo. Arsenal ilijaribu kutunisha misuli, lakini dakika za mwisho pumzi zilikata na kujikuta wakipigwa kikumbo kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo na matokeo yake, kumaliza nafasi ya pili, inayowafanya kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya miaka mingi kupita. Ushindi wa Man United kwa Chelsea umewafanya kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo huo na kukata tiketi ya Ulaya, huku Newcastle wakikamilisha Top Four.
Wababe wengine wa Big Six kama Liverpool, Tottenham na Chelsea zenyewe hazitakuwapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku baadhi yao wakichuana kucheza kwenye Europa League na Europa Conference League. Chelsea msimu wao ulikuwa mbaya zaidi.
Wakati Ligi Kuu England ikifika tamati, kuna mastaa hao wamefanya mambo makubwa kwelikweli na kuachana alama zao kwa maana ya kufunika kwenye baadhi ya maelezo, huku kukiwa na klabu pia ambazo zilikuwa na ubora mkubwa kwenye maeneo fulani na kuzipiku nyingine.
Wanafunga sana
Wanasema raha ya mechi bao. Na hakika kuna wachezaji hao wamelifanya hilo kwa vitendo kwenye Ligi Kuu England msimu huu baada ya kuwa bize kwenye kuhakikisha mipira inatinga kwenye nyavu na kuwafanya mashabiki kupata burudani ya kushangilia mabao. Kuna orodha ya mastaa hao walikuwa tishio kwenye kutikisa nyavu, ikiongoza na straika wa Man City, Erling Haaland, aliyefunga mara 36 na kuandika rekodi mpya kwenye ligi hiyo. Aliyefuatia kwa kufunga mara nyingi ni mkali wa Tottenham, Harry Kane - aliyefunga 28, kisha anafuatia Ivan Toney wa Brentford na mabao yake 20, huku staa wa Liverpool, Mohamed Salah akifunga 19, Callum Wilson wa Newcastle akitupia mara 18 na fowadi wa Man United, Marcus Rashford akitikisa nyavu za wapinzani mara 17.
Wapishi wa pasi za mwisho
Ili mabao yafungwe, kuna ambao walipiga pasi za mwisho kabisa kabla ya mpira hiyo kuwafikia wafungaji. Kwenye soka hiyo inaitwa asisti na hakika kwenye Ligi Kuu England kuna mabingwa wa kupiga asisti. Kwa msimu huu, kiungo gilisi wa Man City, Kevin De Bruyne ndiye aliyepika pasi nyingi za mabao, akifanya hivyo mara 16 na bila ya shaka ataondoka na tuzo msimu huu. Nyuma yake yupo Bukayo Saka wa Arsenal, aliyepiga pasi za mabao 11, sawa na Mo Salah wa Liverpool, huku mkali mwingine wa Man City, Riyad Mahrez na yule wa Crystal Palace, Michael Olise kila mmoja akiasisti mara 10 sawa na Leandro Trossard wa Arsenal. James Maddison wa Leicester City amepiga pasi tisa, kisha wakifuatia wakakali wawili wa Man United, Bruno Fernandes na Christian Eriksen, waliopiga nane kila mmoja.
Muda wote wanautaka
Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, kumeshuhudiwa mastaa waliokuwa wakiutaka mpira muda wote uwe kwenye miguu yao na kufanya kazi ya kusambaza kwa wenzao na hivyo kujikuta wakifunika kwa kupiga pasi nyingi kwa msimu huu. Wakati kila timu ikibakiza mechi moja kuhitimisha msimu huu, kwenye Ligi Kuu England kuna mastaa wamepiga pasi nyingi kuliko wengine. Beki wa Brighton, Lewis Dunk amefunika, akiwa amepiga pasi 3,208. Rodri wa Man City anafuatia kwa kupiga pasi 2,977 kisha anakuja Virgil van Dijk wa Liverpool, aliyepiga pasi 2,581. Gabriel wa Arsenal amepiga pasi 2,33o na kufuatiwa na Pierre-Emile Hojbjerg, aliyepiga pasi 2,256, Trent Alexander-Arnold wa Liverpool pasi 2,235 na Moises Caicedo wa Brighton, amepiga pasi 2,171.
Mikono salama hii
Man United inamlipa David De Gea mshahara wa Pauni 375,000 kwa wiki kutokana na huduma yake anayotoa huko Old Trafford. Na hakika kwa namba za Ligi Kuu England kwa msimu huu, De Gea amekuwa mikono salama kwenye kikosi hicho, akiongoza kwa kucheza mechi nyingi bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa. Kwenye soka zinaitwa Clean Sheets. De Gea amecheza mechi 17 bila ya kuruhusu bao na bila shaka atanyakua tuzo ya Glovu za Dhahabu msimu huu. Alisson Becker wa Liverpool amefuatia na mechi zake 14 bila ya kuruhusu bao sawa na Nick Pope wa Newcastle United. Aaron Ramsdale wa Arsenal akifuatia akiwa amecheza mechi 13 bila ya kuokota mpira kwenye vyavu zake kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Ederson wa Man City ameshuhudia mechi 11 tu alizocheza bila kufungwa.
Umepigwa mpira mwingi
Mashabiki wa soka wanakwenda kutazama mechi uwanjani wakitarajia kuona gongagonga nyingi za kutosha na hakika kwenye Ligi Kuu England kuna timu hizo hazikutana kuwanyima ladha hiyo wapenzi wao baada ya kupiga mpira mwingine uwanjani. Man City imeongoza kwa kupiga gonga nyingi, ikipiga pasi 24,437. Mpira mwingi. Liverpool inafuatia, ikiwa imepiga pasi 21,797 kisha Brighton iliyokuwa kivutia uwanjani kwa kupiga pasi 20,853. Chelsea matokeo hayakuwa mazuri kwao, lakini walivutia kuwatazama, wakipiga pasi 20,556 na kufuatiwa na Arsenal na Man United zilizopiga pasi 1,994 na 18,593 mtawalia. Tottenham wao kwa msimu huu kwenye ligi wamepiga pasi 17,605. Kwa namba hizo, bado imeonyesha Big Six timu zake zinapiga mpira mwingi na bila shaka msimu ujao utakuwa wa kibabe zaidi.
Nyavu zimekoma
Man City wanaendelea na shangwe lao la kubeba taji lao la tatu mfululizo la Ligi Kuu England likiwa la tano katika misimu sita iliyopita wakiwa na kocha Pep Guardiola. Wanastahili baada ya kuzikomesha sana nyavu za wapinzani wao kwenye Ligi Kuu England msimu huu, baada ya wababe hao wa Etihad kufunika kwa mabao, wakifunga mara 94. Kesho wakipiga sita watafikisha 100. Arsenal wamefuatia kwa kukomesha nyavu za wapinzani mara nyingi, wakifunga mara 83 wakifuatiwa na Brighton na Liverpool zilizotupia mipira kwenye nyavu za wapinzani mara 71 kila moja. Newcastle imefunga 68, Spurs 66, Brighton mara 57 na timu isiyokuwa na straika wa maana, Man United imefunga mara 56. Uzuri wa Man City ni kwamba yenyewe imetikisa nyavu wa wapinzani mara nyingi na wao kuruhusu nyavu zao kuguswa mara chache sana.
Hawafungwi hovyo
Man United msimu huu kwenye Ligi Kuu England imeruhusu mabao 42. Timu zilizofungwa mabao machache zaidi yao ni Man City na Newcastle United, ambazo nyavu zimeguswa mara 32 kila mmoja. Man United imeruhusu mabao 42, lakini si mara zote unaweza kupata bao dhidi yao, baada ya kucheza mechi 17 kati ya 37 walizocheza hadi sasa bila ya wavu wao kuguswa. Timu iliyofuatia kwa kuonyesha ugumu wa kuruhusu bao hovyohovyo ni Liverpool na Newcastle, ambao wamecheza mechi 14 kila moja bila ya kuruhusu nyavu zao kutikiswa, wakifuatiwa na Arsenal na Man City, ambazo zimeshuhudia mechi 13 zikicheza kati ya 37 bila ya kuokota mipira kwenye nyavu zao. Aston Villa na Brighton nazo zimekuwa si timu za kuruhusu mabao hovyo, zikicheza mechi 12 bila ya kuruhusu bao.
Mwaga maji tuteleze
Kwenye soka la kisasa, vijana wanaita tukio la kupiga krosi ni kumwaga maji. Kwenye Ligi Kuu England kuna timu zimemwaga maji ya kutosha. Liverpool ni vinara, ikiwa imepiga krosi 772 kwenye mechi 37 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England, wakifuatiwa na Fulham ambao wamepiga krosi 753. West Ham hawapo mbali, wakiwa wamemwaga maji mara 742, wakifuata Man City waliopiga krosi 734, kisha Newcastle United iliyopiga krosi 729 na Spurs krosi 713. Brighton imepiga krosi 687, huku Everton inayopambana isishuke daraja, yenyewe imepiga krosi 674 na Chelsea imechora namba ya maajabu, ikipiga krosi 666. Arsenal imepiga krosi 660, huku jambo hilo likionekana sio mtindo kabisa wa soka la Man United chini ya kocha Erik ten Hag, ambapo timu hiyo ya Old Trafford yenyewe imepiga krosi 504 na kushika namba 18 huko.