Uefa kufanya mabadiliko matatu

Muktasari:
- Muundo huu mpya, awali ulikutana na ukosoaji kutoka kwa mashabiki na wataalamu, hata hivyo, tangu kuanza kwa msimu huu, umepokewa vyema.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kukosoelewa sana kuhusu muundo wao mpya wa Ligi ya Mabingwa, shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA) sasa linataka kufanya mabadiliko ya aina tatu katika mashindano hayo kuanzia msimu ujao.
UEFA ilitangaza mabadiliko makubwa kwa uendeshaji Ligi ya Mabingwa kuanzia msimu wa 2024-25 ambapo idadi ya timu katika mashindano iliongezeka kutoka 32 hadi 36, pia ilianzisha mfumo mpya wa ligi kutoka hatua ya makundi, ambapo timu nane za juu zitaingia moja kwa moja katika hatua ya 16 bora, huku timu zilizomaliza nafasi ya tisa hadi ya 24 zikicheza mechi za mtoano kupata timu nane nyingine zitakazocheza hatua hiyo.
Muundo huu mpya, awali ulikutana na ukosoaji kutoka kwa mashabiki na wataalamu, hata hivyo, tangu kuanza kwa msimu huu, umepokewa vyema.
Lakini sasa UEFA inatarajia kufanya mabadiliko matatu kwenye muundo huo, na moja ya mabadiliko hayo inalenga kupunguza mzigo kwa wachezaji kutokana na ongezeko la mechi.
Kwa mujibu wa gazeti la Kijerumani, BILD, mabadiliko ya kwanza yanayozungumziwa ni kuondoa muda wa ziada, ambapo ikiwa mechi ya mtoano itamalizika kwa sare, itamalizwa kwa mikwaju ya penalti. Mabadiliko ya pili yatakuwa ni kwamba timu zitakazomaliza ndani ya nafasi nane za juu katika hatua ya ligi zitapata faida kwa kupangiwa kucheza mechi ya pili ya mtoano nyumbani.
Muundo wa zamani wa Ligi ya Mabingwa ulizuia uwezekano wa timu mbili kutoka taifa moja kukutana hadi itakapofika hatua ya robo fainali, hata hivyo, jambo hilo halikuwa hivyo msimu huu, kwani Real Madrid ilikutana na Atletico Madrid, huku Bayern Munich ikicheza na Bayer Leverkusen.
Kuelekea msimu ujao kuna uwezekano mfumo wa zamani ukarudi.
Ligi ya Mabingwa ya msimu huu inakaribia kumalizika huku timu nne pekee zikibaki kwenye mashindano, ambazo ni Barcelona, Inter Milan, Arsenal na Paris Saint-Germain zinazotarajiwa kucheza nusu fainali wiki ijayo.