Waarabu watua kwa Onana

Muktasari:
- Kipa huyo wa kimataifa wa Cameroon alionekana mwenye furaha alipojitokeza tena katika kituo cha mazoezi cha Man United cha Carrington, Jumatatu wiki hii, baada ya kupewa muda wa kupumzika na Ruben Amorim ili kutuliza akili yake.
MANCHESTER, ENGLAND: KIPA wa Manchester United, Andre Onana amepewa ofa nono kutimkia Saudi Arabia, lakini amesisitiza kwamba anataka kubaki na kupambania nafasi kikosini.
Kipa huyo wa kimataifa wa Cameroon alionekana mwenye furaha alipojitokeza tena katika kituo cha mazoezi cha Man United cha Carrington, Jumatatu wiki hii, baada ya kupewa muda wa kupumzika na Ruben Amorim ili kutuliza akili yake.
Kocha Amorim hakumjumuisha Onana kwenye kikosi kilichopoteza kwa mabao 4-1 dhidi ya Newcastle wikiendi iliyopita baada ya makosa aliyofanya dhidi ya Olympique Lyon wiki iliyopita.
Hata hivyo, Onana alihakikishiwa kuwa atarejea katika kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Europa League utakaochezwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Kipa namba mbili, Altay Bayindir, mwenye umri wa miaka 27 pia alionekana kuwa na wakati mgumu alipopewa nafasi ya kusimama langoni kwenye mchezo dhidi ya Newcastle United ambapo aliruhusu mabao manne.
Onana, mwenye miaka 29, alionekana akiwa ametulia na mwenye furaha alipowasili mazoezini akiwa na mmoja wa wawakilishi wake, na hata akasimama kwa ajili ya kusaini jezi kwa mashabiki waliokuwa nje.
Staa huyo hivi karibuni amebadilisha wakala, jambo lililozua uvumi kwamba huenda akawa anapanga kuondoka Man United.
Kabla ya kutua Man United akitokea Inter Milan 2023, Onana alikuwa akiwindwa na timu za Saudi Arabia na hadi sasa baadhi zimeendelea kuhitaji huduma yake. Hata hivyo, inaelezwa kuwa hana mpango wa kuondoka kwa sasa kutoka kwa kikosi cha Amorim kinachopitia wakati mgumu, na badala yake anapanga kuwathibitishia wakosoaji wake kuwa wanakosea kumsema vibaya.