Wasaudia waweka mzigo kwa Greenwood

Muktasari:
- Greenwood alijiunga na Marseille katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kwa mkataba wa miaka mitano akitokea Manchester United, na kwa kiasi kikubwa ameonyesha kiwango bora hadi sasa.
MARSEILLE, UFARANSA: MSHAMBULIAJI wa Marseille, Mason Greenwood huenda akatimkia Saudi Arabia katika dirisha la majira ya kiangazi baada ya matajiri hao kuweka mezani Euro 90 milioni kwa ajili ya kuipata huduma yake.
Greenwood alijiunga na Marseille katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kwa mkataba wa miaka mitano akitokea Manchester United, na kwa kiasi kikubwa ameonyesha kiwango bora hadi sasa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 tayari amefunga mabao 17 katika mechi 30 kwenye mashindano yote akiwa na timu hiyo ya Ligue 1, na pia ametoa asisti nne za mabao.
Hata hivyo, hivi karibuni ameingia katika sintofahamu na kocha Roberto de Zerbi ambaye ameweka wazi kwamba hafurahishwi na utendaji kazi wake na ameweka wazi kwamba anaona hajitumi inavyotakiwa.
Ikiwa usajili wake kwenda Saudi Arabia utafanikiwa kwa kiasi tajwa cha pesa kama ilivyoripotiwa na Fichajes, Man United pia itafaidika kwa kupata pesa nyingi kwani katika mkataba wa mauziano kati ya Marseille na Man United kuna kipengele kinachowapa Mashetani Wekundu asilimia 50 ya mauzo.
Hata hivyo, Greenwood mwenyewe bado anatamani kuendelea kusalia katika viunga vya Marseille licha ya nyakati ngumu anazopitia kwani anaamini anaweza kurudisha kiwango chake.