Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Mpenzi Jini’ yamrudisha mjini Z anto

Muktasari:

  • Hivyo ndivyo ilivyo kwa ‘Mpenzi’ maarufu kama ‘Mpenzi Jini’, wimbo wa Z Anto uliotoka miaka 22 iliyopita, ambao sasa umerejea kwa sura mpya baada ya mkongwe huyo kuachia video yake kwa mara ya kwanza.

MPENZI JINI YAMRUDISHA MJINI Z ANTOKUNA nyimbo zinapopita miaka hazifi, badala yake huzidi kupata maisha mapya kila kizazi kinapopata nafasi ya kuzisikiliza.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa ‘Mpenzi’ maarufu kama ‘Mpenzi Jini’, wimbo wa Z Anto uliotoka miaka 22 iliyopita, ambao sasa umerejea kwa sura mpya baada ya mkongwe huyo kuachia video yake kwa mara ya kwanza.

Ni hatua ambayo imekuja kuwashangaza wengi mashabiki zake na wadau wa muziki huku Z Anto anasema alikuwa na mpango tofauti.

Badala ya kuanza na kazi mpya, akaamua kwanza kuifufua ile iliyowahi kutikisa miaka ya nyuma.

Sasa, kazi hiyo imeanza kufanya vizuri, huku ikiwafikia hata wale wa kizazi kipya ambao hawakuwepo wakati wimbo huo ulipotoka.


WAZO LA VIDEO LILIVYOPATIKANA

Z Anto anasema mpango wake wa awali ulikuwa kuachia wimbo mpya, lakini mambo yakabadilika ghafla alipokutana na watu wake wa karibu wakati wa chakula cha jioni.

Wakati wakizungumza, ndipo wenzake walipompelekea wazo la kufanya video ya ‘Mpenzi Jini’ kama surprise kabla hajaanza kutoa kazi mpya.

“Tulikutana kwenye pointi lakini wakanizidi pointi, zikawa na nguvu zaidi na 'idea' waliyonihadithia nikasema hii ngoja tuifanye,” alisema Z Anto.

Kilichofuata hakikuwa kikao cha wiki wala maandalizi ya miezi kwani Kwa mujibu wa Z Anto, siku ya kwanza walijadili wazo hilo, siku ya pili wakatafuta location na siku ya tatu wakaingia kwenye kurekodi video.


VIXEN AKAWA KAMA MTIHANI

Z Anto anasema msichana wa kwanza waliyemtafuta katika mitandao hakutoa majibu yoyote, walimtafuta wa pili ambaye alikuwa tayari kufanya kazi hiyo, lakini gharama zake zikawa juu kidogo.

Hapo ndipo jukumu hilo likahamia kwa marafiki zake na wao ndio waliosimamia maandalizi ya eneo la kurekodia 'location' pamoja na kuhakikisha wanapata idadi ya watu waliohitajika kabla Z Anto hajaingia rasmi kurekodi video.

Kwa upande wa bajeti, Z Anto hakutaka kuweka wazi kiasi halisi alichotumia, lakini anaeleza video hiyo imetumia fedha nyingi.

"Siku hizi hakuna video rahisi. Kuna wasanii wanafanya video za hadi milioni 40 ili kupata uhalisia unaoendana na soko," anasema Z Anto


MPENZI JINI HAKUWA MTU WA KWELI

Kwa miaka yote, jina ‘Mpenzi Jini’ limeweza kumfanya msikilizaji kujiuliza kama kulikuwa na tukio la kweli nyuma ya wimbo huo.

Hata hivyo, Z Anto anasema stori hiyo haikutokana na maisha yake binafsi, bali ilikuwa ni ubunifu wa kiuandishi uliotengenezwa kutokana na mazingira ya ushindani wa muziki yaliyokuwepo wakati huo.

“Haikuwa stori ya maisha yangu. Ilikuwa ni uandishi wa stori tu kutokana na mazingira ya ushindani wa muziki wakati huo,” anasema Z Anto.


UANDISHI WA "MPENZI JINI"

Cha kushangaza zaidi ni namna wimbo huo ulivyoandikwa, Z Anto anasema mstari wa kwanza aliandika ndani ya dakika chache, lakini baada ya hapo hakukimbilia kuumaliza.

Aliibeba vesi hiyo kwa takribani mwezi mmoja bila kuandika nyingine baadaye aliporudi kuendelea na kazi hiyo, ya pili nayo iliandikwa ndani ya muda mfupi na hatimaye wimbo ukakamilika. Kuanzia hapo ‘Mpenzi Jini’ ikawa sehemu ya historia yake na sasa, baada ya miaka 22, inapata nafasi nyingine katika video.


MIAKA 30 YA BONGO FLAVA YAMWAMSHA

Kwa Z Anto, kurejea kwenye muziki hakukutokea kwa bahati tu kwani miaka 30 ya Bongo Flava ilimpa msukumo na kumrudisha kwenye hisia za muziki, lakini uamuzi wa kufanya video ya ‘Mpenzi Jini’ ulisukumwa zaidi na marafiki zake.

Watu hao, kwa mujibu wake, waliona upande wa kibiashara wa wazo hilo na wakamsukuma kulitekeleza.

Sasa, uamuzi huo umeanza kuzaa matunda. Video imeanza kufanya vizuri ikiwa na watazamaji 540k kwenye mtandao wa YouTube na kumrudisha Z Anto kwenye muziki, huku wimbo ukianza kufika hata kwa kizazi ambacho hakikuwahi kuupitia wakati ulipotoka.


NGOMA MPYA IPO NJIANI

Anaweka wazi mashabiki zake wakae tayari kwa ngoma mpya, ambayo anaweza kuiachia muda wowote kuanzia sasa.

Pia aliomba kuendelea kufuatilia kurasa zake za Instagram, TikTok na YouTube, kwa sababu bado ana supraizi nyingine anazozipanga.

Kwa hiyo, miaka 22 baada ya ‘Mpenzi Jini’ kuingia kwenye masikio ya mashabiki, Z Anto amerudi na video ambayo imefungua mlango wa kumbukumbu za zamani huku ikimpeleka moja kwa moja kwenye kizazi kipya.