Eliud kuisimamisha Mbeya na shoo ya Makuzi
Muktasari:
- Shoo hiyo inatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa City Park jijini humo, akisindikizwa na wasanii wengine, huku zaidi ya watu 2,000 wakitarajiwa kushiriki tukio hilo litakaloambatana na maisha ya mchekeshaji huyo maarufu nchini.
MBEYA, MCHEKESHAJI Eliud Samuel anatarajia kuisimamisha Jiji la Mbeya atakaposimama jukwaani kuwavunja mbavu wadau na mashabiki wa sanaa kupitia shoo maalumu ya ‘Makuzi’ itakayofanyika Desemba 24, mwaka huu.
Shoo hiyo inatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa City Park jijini humo, akisindikizwa na wasanii wengine, huku zaidi ya watu 2,000 wakitarajiwa kushiriki tukio hilo litakaloambatana na maisha ya mchekeshaji huyo maarufu nchini.
Akizungumza leo, Agosti 21, jijini Mbeya, Samuel amesema ameamua kuleta shoo hiyo maalumu kwa wakazi wa Mbeya kwa kuwa ndipo nyumbani ambapo ataelezea historia ya maisha yake kuanzia malezi hadi makuzi.
Amesema shoo hiyo ya kwanza kufanyika jijini humo itawashirikisha baadhi ya wasanii wakubwa, japokuwa atasimama mwenyewe zaidi jukwaani kwa kuwa ataitumia siku hiyo kuelezea safari yake na maisha kwa ujumla.
“Ndio maana leo nimetangaza shoo hii kupitia Shule ya Sekondari Nzondahaki niliyosoma, hivyo shoo hii itakuwa maalumu kwa ajili ya kuelezea safari yote ya maisha yangu kuanzia malezi hadi makuzi,” amesema Samuel.
Hata hivyo, mvunjambavu huyo alitumia nafasi hiyo kukabidhi vifaa vya michezo kwa wanafunzi na vitendea kazi kwa walimu wa shule ya sekondari Nzondahaki aliyosoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Miongoni mwa vifaa alivyokabidhi ni jezi, mipira, meza, kompyuta, mabegi, vifaa vya matangazo ‘muziki’ na vipaza sauti, akilenga kuhamasisha vipaji na kuchochea mazingira mazuri ya ufundishaji shuleni hapo.
Kwa upande wake, Friday Kyando amesema matarajio yao ni kushirikisha zaidi ya watazamaji 2,000 akieleza kuwa kwa sasa maandalizi yanaendelea vyema akitoa shukrani kwa wadau waliosapoti tukio hilo.
“Hii ni maalumu kwa Samuel kuelezea safari ya maisha yake, kuhusu viingilio itatangazwa rasmi bada ya mwezi mmoja kwakuwa kwa sasa tupo bado hatua za awali, tunawakaribisha wadau wenye utayari kushirikiana na sisi,” amesema Kyando.
Mkuu wa shule ya sekondari Nzondahaki, Reinfrid Hyera ameshukuru msaada huo akiomba wasanii na wadau wengine kuikumbuka shule hiyo ambayo iliwapa elimu hadi kufikia malengo yao.
“Vifaa hivi kwanza vitaongeza hamasa na chachu katika ufundishaji, lakini hata wanafunzi watahamasika sana katika kupenda vipaji vyao, wanapokuja watu maarufu shuleni hapa ni faida kwa maisha ya baadaye kwa watoto” amesema Hyera.