Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauthar anavyotembea na taarabu

KAUTHAR Pict

Muktasari:

  • Kwenye harakati hizo yupo Kauthar Hassan, binti wa Zanzibar ambaye ndani ya mwaka mmoja uliopita ameanza kupata umaarufu mkubwa kupitia sauti yake, staili yake ya kuimba na nyimbo zinazowafikia watu wa rika tofauti.

ZILIPITA siku ambazo Taarabu ilionekana kusubiriwa zaidi na watu wa kizazi fulani, lakini sasa sauti yake inarudi mitaani, safari hii ikiwa na ladha inayowagusa zaidi Gen Z.

Kwenye harakati hizo yupo Kauthar Hassan, binti wa Zanzibar ambaye ndani ya mwaka mmoja uliopita ameanza kupata umaarufu mkubwa kupitia sauti yake, staili yake ya kuimba na nyimbo zinazowafikia watu wa rika tofauti.


KAU 01

AKUOGOPE NANI YAMFUNGULIA NJIA

Kauthar amekuwa kwenye muziki kwa takribani miaka saba, lakini anasema mwaka mmoja uliopita ndiyo mambo yalianza kwenda kwa kasi baada ya kazi zake kuanza kukubalika zaidi. Akizungumza mahojiano na Mwanaspoti, mwanamuziki huto anasema kipaji chake alikigundua akiwa Kidato cha Pili.

Anakumbuka siku walimu walipomuuliza ndoto yake, alijibu kwa ujasiri kuwa anatamani kuwa muimbaji mkubwa, jambo lililofanya kila mtu darasani amcheke na kumshangaa. Mtu aliyemshika mkono na kumpa ujasiri alikuwa dada yake, Mariam, ambaye ndiye aliyekuwa akifanya naye mazoezi ya kuimba kwenye baraza la nyumbani.

Kutoka kwenye mazoezi hayo ya kawaida, Kauthar alipata ujasiri wa kwenda kwenye usaili na kuanza safari yake rasmi ya muziki.

Kauthar alisema umaarufu wake ulizidi kupitia wimbo ‘Akuogope Nani’ kwani umefikisha wasikilizaji zaidi ya milioni moja kwenye mtandao wa YouTube. Wimbo huo ulianza kusikika kwa kasi na kumfanya akubalike kwa watoto, vijana, wadada, wakaka na hata wazee.

“Wimbo wangu wa Akuogope Nani, hakuna mtu ambaye haichezi. Nina uhakika kwamba hiyo ndiyo nyimbo yangu ya kwanza ambayo imesababisha mpaka leo hii nikawa Kauthar Hassan,”  anasema Kauthar.

Wimbo huo ulipata umaarufu kupitia mitandao ya kijamii kama TikTok, wengi walikuwa wakifanya chalenji za wimbo huo na kwenye shughuli mbalimbali mitaani kama harusi, umekuwa ukisikika sana.


KAU 02

TAARABU HAIJAFA

Kauthar anasema hakubali kabisa kauli kwamba Taarabu imepoteza mvuto.

Kwa upande wake, muziki huo bado una nafasi kubwa, ila wasanii wanapaswa kujua mashabiki wa sasa wanataka nini.

“Taarab haijafa na haiwezi kufa, sisi tufa na tutahakikisha kwamba inasimama na inaendelea kusimama,” anasema Kauthar.

Anasema moja ya sababu zinazomfanya awafikie vijana ni namna anavyoiweka Taarabu yake bila kuiacha kabisa misingi yake.

Mistari, michambo na staili yake ya uimbaji vimeanza kumuingiza kwenye masikio ya Gen Z, kundi ambalo mara nyingi limekuwa likihusishwa zaidi na Bongo Fleva na muziki wa kizazi kipya.


KAU 03

MUME, MENEJA NA BOSI

Nyuma ya safari hiyo yupo Shaaban Salumu, maarufu Shebby Kinanda ambaye ni mume wa Kauthar, meneja wake na pia bosi wa bendi anayofanyia kazi ambayo ni Shebby Kinanda Classic Band.

Kauthar hamfichi Shebi kwenye mafanikio yake, kwani amekuwa mtu muhimu tangu mwanzo, akimsaidia kwenye mazoezi, matumizi ya pumzi na kumfundisha mambo mbalimbali kuhusu muziki wa Taarabu.

“Yeye ndiyo nguzo yangu kwanza, kwa sababu kama si yeye nisingefika kokote,” anasema Kauthar.

Kauthar anasema anafanya kazi na bendi yake ya kudumu, tofauti na baadhi ya wasanii wanaozunguka sehemu mbalimbali kufanya maonyesho.

Hata hivyo, safari haikuwa laini kila wakati. Anasema kuna kipindi aliwahi kufikiria kuacha muziki baada ya baadhi ya nyimbo zake kutofanya vizuri, lakini sasa anaona mambo yameanza kubadilika.


KAU 04

TAARABU YA LEO INA TATIZO

Kauthar anapenda Taarabu, lakini changamoto zipo ndani yake.

Anasema kuna bendi nyingi Zanzibar, Pemba na Tanzania Bara, lakini baadhi yake zimekuwa zikikosa maudhui yenye uzito.

Kwa kwake, Taarabu si kelele za muziki pekee, bali ni ujumbe unaoweza kumfanya mtu acheke, alie au aketi chini na kutafakari.

Katika kuwatazama waliomtangulia, anawapa heshima wakongwe kama Kija Kosa kwa uchangamfu wake na Rukia Ramadhani kwa ufundi wa mianguko na mikia ya sauti.


KAU 05

MWANGA HUU HAPA, LAKINI BADO

Kauthar anasema mafanikio ya sasa hayamaanishi kwamba ameshafika mwisho wa safari.

“Kwangu mimi nimeona mwanga, kama ni asubuhi basi nimeanza kuiona ile saa 11, ila bado sijafika, lakini naamini ipo siku itakuwa vizuri,” anasema Kauthar.

Kauli hiyo inaonyesha bado ana kiu ya kwenda mbali zaidi na Taarabu yake.


MASHABIKI KILA KITU

Kwa mashabiki waliompa nafasi, Kauthar anasema hataki umaarufu umbadilishe alivyo akiwaomba waendelee kumpa upendo huo huo na kumkumbuka kama mtu mwenye roho safi.

Na kama siku moja Mwenyezi Mungu atamfikisha kwenye mafanikio makubwa zaidi, anasema hataki kutumia nafasi hiyo kwa ajili yake pekee, bali kuwasaidia wenye uhitaji.

“Kitu kikubwa ambacho nakiishi siku zote za maisha yangu ni upendo wangu huu huu ambao mimi ninao kwa mashabiki zangu na wao wanao kwangu. Mwenyezi Mungu akinifikisha, basi nitabeba shida ya mtu yeyote yule,” anasema.

Kauthar Hassan bado hajafika mwisho, lakini tayari ameanza kuacha alama. Sauti yake ikiendelea kusikika!