Wako moto! Elversberg ni kina nani?
Muktasari:
- Miaka zaidi ya minne iliyopita, Elversberg walimaliza kileleni mwa Regionalliga Sudwest, mojawapo ya ligi za daraja la nne nchini Ujerumani. Elversberg walikuwa wakicheza katika ligi ya kanda iliyokuwa ikijumuisha timu kutoka kusini magharibi mwa nchi hiyo na sasa wamepiga hatua kubwa tangu wakati huo kupitia uwanja wao wa Waldstadion an der Kaiserlinde, ambao kwa sasa una uwezo wa kuchukua watazamaji 10,000 na unatarajiwa kufikia 15,000 baada ya kazi za ukarabati kukamilika.
MUNICH, UJERUMANI: BAADA ya kupanda kwa kiwango cha kushangaza Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), Elversberg wameanza msimu wao wa kwanza kwa ushindi mara mbili, sare moja na kipigo kimoja cha dakika za lalasalama walipoikaribisha Bayern Munich. Lakini, hii ndiyo simulizi yao.
Miaka zaidi ya minne iliyopita, Elversberg walimaliza kileleni mwa Regionalliga Sudwest, mojawapo ya ligi za daraja la nne nchini Ujerumani. Elversberg walikuwa wakicheza katika ligi ya kanda iliyokuwa ikijumuisha timu kutoka kusini magharibi mwa nchi hiyo na sasa wamepiga hatua kubwa tangu wakati huo kupitia uwanja wao wa Waldstadion an der Kaiserlinde, ambao kwa sasa una uwezo wa kuchukua watazamaji 10,000 na unatarajiwa kufikia 15,000 baada ya kazi za ukarabati kukamilika.
Hadi hapo, uwanja huo utaweza kuchukua kila mtu kutoka katika manispaa ndogo ya Spiesen-Elversberg, iliyopo upande wa kaskazini-mashariki kidogo mwa Saarbrücken, yenye wakazi takribani 13,000 tu. Elversberg walipata nafasi ya kupanda daraja kwa mara ya pili mfululizo msimu wa 2022-23, na kufika Ligi Daraja la Pili Taifa Ujerumani. Kwa Bundesliga hii ni mara ya kwanza katika historia yao.
Wakali hao wangeweza kupanda Bundesliga mapema zaidi, lakini walifungwa kwa jumla ya mabao 4-3 na Heidenheim katika mechi za mchujo za kupandisha daraja msimu wa 2024-25. Hata hivyo, walirekebisha hilo mwaka mmoja baadaye, wakimaliza nafasi ya pili nyuma ya Schalke, huku wakiwa mbele ya Paderborn iliyomaliza nafasi ya tatu kwa tofauti ya mabao na hivyo kupata nafasi ya kupanda moja kwa moja. Ilikuwa hatua kubwa kupanda daraja, na ratiba ilipotoka, kuona kwamba mechi zao mbili za kwanza zingekuwa dhidi ya klabu mbili kubwa zaidi nchini Ujerumani huenda lilikuwa jambo la kusisimua na la kutisha kwa kiwango kikubwa. Mechi ya kwanza ya Elversberg katika Bundesliga ilikuwa dhidi ya Bayer Leverkusen, ambao walitwaa ubingwa miaka miwili iliyopita.
Kama walikuwa na hofu, basi vijana hao wapya hawakuionyesha. Walifunga mabao mawili ndani ya dakika tisa tu kupitia Lukas Petkov na Cole Campbell, kisha David Mokwa akaongeza la tatu muda mfupi baada ya mapumziko. Kwa kuwa hiyo ilikuwa ligi ya juu kabisa, mambo hayakuwa rahisi hivyo kwao. Patrik Schick alipunguza bao na Christian Kofane akafanya mwisho wa mchezo kuwa wa presha kwa kufunga jingine katika muda wa nyongeza, lakini wenyeji walishikilia ushindi na kurekodi ushindi wao wa kwanza katika Bundesliga.
Baada ya mchezo Elversberg walijikuta wakianza kuzungumziwa zaidi na mashabiki pamoja na wadau wa soka mitaani nchini humo. Lakini, kama mechi hiyo ilikuwa ya kusisimua kilichofuata katika mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Borussia Monchengladbach ilikuwa kama tukio lililotoka kwenye filamu.
Baada ya dakika 56 katika Uwanja wa Borussia-Park, Elversberg walikuwa nyuma kwa mabao 3-1. Hapo ndipo ilipoonekana hali halisi, kwani waliokuwa wamepanda daraja kwa mara ya kwanza walikuwa wakionjeshwa jinsi Bundesliga ilivyo ngumu kwa wageni na kupata somo la kile kinachohitajika kucheza katika kiwango cha juu. Kisha mabao ya Maurice Krattenmacher na Felix Keidel yaliwasawazishia mambo kwa namna ya kushangaza, Krattenmacher kuifungia Elversberg bao la ushindi katika muda wa nyongeza.
Elversberg wakawa timu ya sita pekee katika historia ya Bundesliga, ukiondoa msimu wa kwanza wa 1963-64, na ya pili tu tangu mwanzo wa karne hii kushinda mechi mbili za kwanza kabisa katika Bundesliga.
Kwa sasa ni moja kati ya timu nne pekee za Bundesliga ambazo zilikuwa na rekodi ya asilimia 100 baada ya mechi mbili kiasi cha kujikuta wakiwa juu ya Bayern Munich kwenye msimamo baada ya mabingwa hao kutoka suluhu dhidi ya Schalke mapema tu. Kwa sasa Elversberg wanashika nafasi ya nane wakiwa na pointi saba katika mechi nne baada ya kufunga mabao manane (likiwamo moja dhidi ya Bayern Munich mechi ya mwisho kabla ya kalenda ya Fifa kwa timu za taifa majuzi), imefungwa saba ikishinda mechi mbili, sare moja na kichapo kimoja (cha 2-1 kutoka kwa Bayern).
HUKO NYUMA
Mwanzoni mwa msimu wa 2022-23, Elversberg walikuwa wakishika nafasi ndani ya 2,000 bora katika viwango vya timu bora duniani, lakini kuonyesha ukubwa wa maendeleo yao tangu wakati huo, sasa wako nafasi ya 130 baada ya ushindi dhidi ya Borussia Monchengladbach, wakiwa juu ya timu kama Wolves ya England na Fiorentina ya Italia.
Kama ilivyo kwa simulizi nyingi za hivi karibuni za klabu zilizokuwa dhaifu na kupanda madaraja, Elversberg wamejijenga kwa kuwa na vipaji vidogo, hata kama ni kwa muda mfupi. Nick Woltemade alitumia msimu wa 2022-23 kwa mkopo hapo akitokea Werder Bremen; Fisnik Asllani alikuwapo kwa mkopo 2024-25 kabla ya kutimkia Hoffenheim; na nyota mpya wa Eintracht Frankfurt, Younes Ebnoutalib, alikuwa gumzo Elversberg katika nusu ya kwanza ya msimu uliopita kabla ya kuondoka. Ebnoutalib alifunga mabao 12 katika mechi 17 za ligi kabla ya kuondoka Januari, lakini Elversberg waliendelea na kasi bila yeye.
Huenda wasiwe na mchezo wa moja kwa moja kila wakati, lakini Elversberg wanapiga pasi ndefu chache zaidi na katika Ligi Daraja la Pili msimu uliopita walizipiga mara 1,537 na bado wanapenda kufanya hivyo hata sasa. Pia wana uwezo mzuri katika mipira iliyokufa, ambapo msimu uliopita walifanya hivyo mara 10, huku wakiwa kati ya timu tatu zilizoruhusu mabao machache (manne) yakitokana na kona.
Licha ya kuwa na vijana wenye akili kubwa, wana kikosi chenye uwiano mzuri. Wastani wa umri wa wachezaji waliotumika katika Bundesliga ni miaka 25 na siku 248. Kuna kina Campbell, Mokwa na Francis Onyeka wanaotesa vizuri wakisaidiana na wenye uzoefu kama Maximilian Rohr, Jan Gyamarah na Luca Schnellbacher.