Pamotoo! Ballon d’Or 2026 ilivyoanika ‘udhaifu’ washambuliaji EPL
Muktasari:
- Ni katika nchi hiyo ambako kuna mastaa bora wa kizazi cha sasa cha soka wanapopishana kutoka pande mbalimbali za dunia, na ni hao ambao wamekuwa wakiibeba ligi hiyo na kuipa umaarufu huku pia timu 20 zinazoshiriki michuano hiyo zikiwa miongoni mwa maarufu zaidi ukiachana na Barcelona na Real Madrid za Hispania, bayern Munich ya Ujerumani na Monaco, Marseille na PSG za Ufaransa.
PARIS, UFARANSA: JUMATATU usiku, Oktoba 26, mwaka huu, zile tuzo za mchezaji bora Ulaya za Ballon d’Or 2026 zitatolewa katikati mwa Jiji la London kule England, ambako ndiko ilipo ligi maarufu zaidi ya soka duniani kwa sasa maarufu kama EPL.
Ni katika nchi hiyo ambako kuna mastaa bora wa kizazi cha sasa cha soka wanapopishana kutoka pande mbalimbali za dunia, na ni hao ambao wamekuwa wakiibeba ligi hiyo na kuipa umaarufu huku pia timu 20 zinazoshiriki michuano hiyo zikiwa miongoni mwa maarufu zaidi ukiachana na Barcelona na Real Madrid za Hispania, bayern Munich ya Ujerumani na Monaco, Marseille na PSG za Ufaransa.
Lakini wiki hii walipotangazwa mastaa 30 wanaowania tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu mshtuko ulihamia katika EPL ambako hakuna washambuliaji wengine waliojitokeza katika orodha hiyo na hilo likaibua mjadala kulikoni ligi maarufu ikakosa watu wakali wanaotakiwa kufunga mabao katika tuzo hizo?
Hata hivyo, yamekuwapo majibu lakini ambayo hata hivyo huenda hayaakisi uhalisia, kwani wachezaji wa safu ya hiyo kutoka EPL hawajawakilishwa vizuri kwenye orodha hiyo, jambo linaloakisi msimu uliotawaliwa na mipira iliyokufa na mipambano ya nguvu, lakini msimu wa 2026-27 tayari unaonekana kuwa na matumaini zaidi eneo la ushambuliaji.
Uwakilishi wa EPL ni mdogo linapokuja suala la wachezaji 16 wa kushambulia walioteuliwa kwenye orodha ya mwaka huu ya Ballon d’Or. Bruno Fernandes wa Manchester United na Erling Haaland wa Manchester City wamo, lakini Cole Palmer, ambaye alikuwa miongoni mwa walioteuliwa mwaka 2025 hayupo baada ya msimu uliokumbwa na majeraha upande wake.
Mwelekeo wa soka la England kuelekea kwenye nguvu za mwili na mipira iliyokufa msimu uliopita unaonekana wazi kutokana na kutokuwepo kwa mshambuliaji yeyote kutoka timu bora nchini humo kwenye orodha hiyo.
Watatu wanaoiwakilisha Arsenal kina Gabriel Maghalhaes, Declan Rice na William Saliba wote wanaelemea zaidi katika majukumu ya ulinzi. Arsenal walitwaa ubingwa wa ligi, lakini washambuliaji wao hawaonekani kuwa katika viwango vya juu kabisa. Majeraha yalichangia hali hiyo, yakimzuia Martin Odegaard, Kai Havertz na Bukayo Saka kupata mwendelezo mzuri, lakini pia Arsenal ya Mikel Arteta haikupendwa na watazamaji wasioegemea upande wowote.
Kulikuwa na heshima zaidi kuliko kuvutiwa na uimara wao wa ulinzi. Kulikuwa pia na hoja kwamba ukosefu wa dhamira ya kushambulia baada ya Arsenal kuongoza bao 1-0 ulioifanya ishindwe kuifunga PSG katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ilikuwa vita iliyokuwa na tofauti ndogo, lakini PSG kutwaa taji la pili mfululizo la Ulaya ulikuwa ushindi wa soka la kushambulia dhidi ya soka la kusukumana la Ligi Kuu England.
Kikosi cha kocha Luis Enrique kinaendelea kuzifunga timu za England, na hali kama hiyo ilionekana pia kwenye Kombe la Dunia 2026. Mechi zilikuwa na mtiririko mzuri zaidi Amerika Kaskazini, kwa sehemu kutokana na waamuzi kuchukua hatua kali dhidi ya kile kilichoitwa mipira iliyokufa.
Kwa upande wa England, mpango wa kocha Thomas Tuchel kutumia faida ya nguvu za kimwili za wachezaji wanazozitumia katika EPL ulishindwa kufanya kazi. England walipotea na kufungwa kwao kwenye nusu fainali dhidi ya Argentina kulimaanisha mambo magumu kwao.
Pia ni muhimu kwamba hadi Anthony Gordon alipofunga dhidi ya Argentina, hakukuwa na mshambuliaji wa England aliyekuwa akicheza EPL msimu uliopita aliyefunga bao kwenye Kombe la Dunia 2026.
Na akizungumza wakati huo siku chache baada ya kuondoka Newcastle United kwenda Barcelona, Gordon alisema: “Soka la Hispania linahitaji kiwango tofauti cha uelewa wa mbinu na ufundi. England, wakati mwingine nguvu na kasi vinaweza kuficha makosa. Unaweza kushindwa kuudhibiti mpira vizuri, lakini bado ukarekebisha kosa hilo kwa kushinda pambano linalofuata la nguvu za kimwili.”
KWANI IKOJE?
Mvuto wa Ligi Kuu England kwa sehemu unatokana na sifa hizo za mipambano mikali ya kimwili, lakini msukosuko huo ulikwenda mbali sana msimu uliopita. Unaweza kukumbuka mechi ngapi za kiwango cha juu? Baadhi ya timu kubwa kuwa na misimu ya kukatisha tamaa hakukusaidia, lakini kwa ujumla kulikuwa na malalamiko kuhusu utegemezi mkubwa wa mipira iliyokufa na makipa kusukumwa au kuzuiwa wakati wa mipango tata ya kupiga kona.
Anthony Barry, msaidizi wa Tuchel, alisema mechi zilikuwa zimejaa msongamano wa wachezaji katikati ya viwanja, na kulikuwa na msisitizo wa mipira mirefu kutoka kurusha pembeni na kupoteza muda, hivyo ligi ilikuwa ngumu kuitazama.
KUNA MWELEKEO?
Sasa mabadiliko yanaanza. Moja ya mambo yaliyojitokeza katika wiki tatu za kwanza za msimu ni kasi ya mchezo kuongezeka. Watunga kanuni wamechukua hatua. Hesabu ya kuchelewesha mpira ya sekunde tano na tishio la kurudisha mchezo nyuma kwenye mipira ya kuanzisha kutoka kwa makipa na ya kurusha pembeni zimezilazimisha timu kufikiria mara mbili kabla ya kupoteza muda.
Ukomo wa sekunde 10 kwa wachezaji wanaotoka uwanjani wakati wa mabadiliko umesaidia, na jaribio la kutumia muda maalumu wa mbinu linamaanisha kwamba mchezaji uwanjani atalazimika kutoka kwa angalau dakika moja baada ya mchezo kuanzishwa upya ikiwa kipa wa timu yake ataanguka chini kutokana na jeraha.
Bila shaka, bado ni mapema, lakini soka limekuwa la kufurahisha na takwimu zinatia moyo. Msimu huu kumekuwapo na mechi nne ambazo timu zote mbili zilipiga mashuti 14, ikilinganishwa na mechi moja pekee katika hatua kama hiyo msimu uliopita.
Kwa mujibu wa Opta, wastani wa muda ambao mpira ulikuwa ndani ya mchezo umeongezeka kutoka dakika 55 na sekunde 23 katika msimu wa 2025-26 hadi dakika 57 na sekunde 14. Muda wa ucheleweshaji umeshuka kutoka sekunde 29.2 hadi sekunde 26.7. Ukiondoa penalti, asilimia ya mabao yanayotokana na mipira iliyokufa imeshuka kutoka asilimia 27.5 hadi asilimia 23.5. Pia, kuna mashambulizi ya haraka zaidi kwa kila mchezo, 2.27 ikilinganishwa na 1.94, mashuti mengi zaidi kwa kila mchezo yanayotokana na mashambulizi hayo, 1.9 ikilinganishwa na 1.75, na mabao mengi zaidi kwa kila mchezo kutokana na mashambulizi ya haraka, 0.43 kutoka 0.23.
Chelsea, ambao wamekuwa wakicheza mpira laini wenye nguvu chini ya kocha Xabi Alonso, wamekuwa wakicheza kwa kasi na wamehusika katika baadhi ya mechi zenye matukio mengi. Liverpool wameachana na Arne Slot na kumleta Andoni Iraola anayesisitiza mashambulizi ya kusisitiza.
Newcastle United wamekuwa na kasi chini ya kocha Matthias Jaissle, ambaye anatumia vizuri uwezo wa Harvey Barnes na Anthony Elanga, huku Roberto De Zerbi wa Spurs anaonekana kuwa tofauti akipambania spidi na kutaka wachezaji wake wacheze soka la kasi.
Nayo Manchester City huenda hivi karibuni wakawa na makali zaidi, kwani kocha wao Enzo Maresca anapendelea mtindo wa taratibu, lakini hata Pep Guardiola alikuwa akiondoka kwenye udhibiti wa kupita kiasi msimu uliopita akisisitiza katika spidi.
Kuna hisia kwamba baadhi ya makocha kwa sasa wako karibu zaidi kimtindo na Jurgen Klopp kuliko Guardiola. Mtindo wa Alonso hadi sasa unaonekana kufanana sana na wa Klopp. Utayari wake wa kuwaacha wachezaji wenye vipaji wacheze kwa uhuru pia unafanana kwa kiasi fulani na Carlo Ancelotti; Palmer akisema ameruhusiwa uhuru zaidi wa kuzunguka uwanjani chini ya Alonso.
Huenda mabadiliko hayo yakatupa vitu vitamu kadiri timu zinavyozoea mbinu za makocha, mashindano ya Ulaya yanapoanza na majeraha yatakapoanza kuathiri vikosi. Huenda ikafurahisha kusikia kwamba Arsenal inaongoza kwa kuchelewesha mchezo wakati wa kona, ikiwa na wastani wa sekunde 43.2.
PICHA LITAKUWAJE?
Hili ni jambo muhimu kwa sasa wakati mastaa wa Ligi Kuu England watakuwa wanawazia kuanza upyaa huku wakijenga taswira ya Ballon d’Or 2027. Florian Wirtz, nyota wa zamani wa Bayer Leverkusen iliyobeba ubingwa chini ya Alonso yupo England, lakini amekuwa akipata ugumu wa kasi ya mchezo Liverpool.
Washambuliaji watatu wa Bayern Munich waliopo kwenye orodha ya Ballon d’Or kina Harry Kane, Luis Díaz na Michael Olise walitoka katika timu za England na ndicho Wirtz na wenzake wapaswa kufanya. Ousmane Dembele na Khvicha Kvaratskhelia wa PSG wanafika katika hatua muhimu ya Ligi ya Mabingwa wakiwa na nguvu kwa kiasi fulani kwa sababu hawalazimishwi kufikia kiwango chao cha juu kila wiki na timu kama Brentford na Bournemouth.
Jude Bellingham, kipaji kikubwa cha England, hajawahi kucheza EPL. Msimu uliopita Vinicius Junior alifikiria kuhamia Arsenal, lakini aliamua kubakia Real Madrid pamoja na Kylian Mbappe.
EPL ndiyo ligi yenye nguvu na ushindani mkubwa zaidi Ulaya. Hata hivyo, kumekuwapo na upotevu wa vipaji. Ni rahisi kufikiria kwamba washambuliaji bora wanahisi watakuwa na furaha zaidi kutengeneza nafasi na kufunga mabao dhidi ya safu za ulinzi za Bundesliga zisizo na presha kubwa, huku pia wakibaki na nguvu za kutosha kushindana katika Ligi ya Mabingwa, mashindano ya kimataifa na kuwania tuzo binafsi. Angalia jinsi timu nne zilizofika nusu fainali ya Kombe la Dunia zilivyokuwa na uwakilishi mkubwa wa mabeki na viungo wa ulinzi kutoka EPL, lakini siyo wachezaji wa pembeni na washambuliaji. Nyota wako wapi? Wale walioondoka hawajabadilishwa kikamilifu, ndiyo maana EPL inaweza kufaidika ikiwa Bradley Barcola atawaka akiwa Liverpool baada ya kujiunga akitokea PSG.
Barcola akifanikiwa anaweza kuwashawishi wengine kumfuata. Lakini kama winga huyo wa Ufaransa atachopotea mapema kutokana na mzigo wa ligi hiyo, inaweza kuwa na athari. EPL inapaswa kuwa makini. Hatua mpya za kukabiliana na kupoteza muda zinaweza kubadilisha mchezo. Kulikuwa na dakika nne pekee za nyongeza mwishoni mwa kila kipindi wakati Arsenal ilipoifunga Chelsea majuzi. Ilikuwa hali yenye kuburudisha.