Keffe D apatikana na hatia mauaji ya Tupac
Muktasari:
- Davis, mwenye umri wa miaka 63, alikutwa na hatia ya mauaji kwa kutumia silaha ya moto, huku majaji 12 wakifikia uamuzi huo jana Jumatatu, Agosti 31, 2026, baada ya kujadili kesi hiyo kwa takribani saa tatu.
BAADA ya takribani miaka 30 ya fumbo lililogubika kifo cha mwanamuziki nguli wa Marekani, Tupac Shakur, hatimaye mahakama imetoa hukumu dhidi ya Duane “Keffe D” Davis baada ya kupatiakana na hatia ya kuhusika katika kupanga mauaji ya msanii huyo.
Davis, mwenye umri wa miaka 63, alikutwa na hatia ya mauaji kwa kutumia silaha ya moto, huku majaji 12 wakifikia uamuzi huo jana Jumatatu, Agosti 31, 2026, baada ya kujadili kesi hiyo kwa takribani saa tatu.
Kwa mujibu wa tovuti ya PEOPLE, hukumu hiyo imekuja ikiwa zimesalia siku chache kutimia miaka 30 tangu Tupac aliposhambuliwa kwa risasi jijini Las Vegas, Septemba 7, 1996.
Tupac, ambaye alikuwa na umri wa miaka 25 wakati huo, alipigwa risasi akiwa ndani ya gari aina ya BMW lililokuwa likiendeshwa na Marion “Suge” Knight, mmoja wa watu mashuhuri katika historia ya muziki wa hip-hop na mwanzilishi wa Death Row Records.
Gari hilo lilishambuliwa na watu waliokuwa ndani ya gari aina ya Cadillac nyeupe, huku Tupac akiwa amekaa upande wa mbele. Alijeruhiwa vibaya na kufariki dunia siku sita baadaye, Septemba 13, 1996.
Ugomvi uliosababisha mauaji hayo!
Kabla ya shambulio hilo, Tupac na watu waliokuwa pamoja naye walihusika katika ugomvi ndani ya Hoteli ya MGM Grand, Las Vegas, baada ya pambano la bondia Mike Tyson.
Katika tukio hilo, Orlando “Baby Lane” Anderson, ambaye alikuwa mpwa wa Keffe D, alipigwa na kundi lililokuwa pamoja na Tupac. Waendesha mashtaka waliieleza mahakama kuwa shambulio dhidi ya Anderson lilikuwa chanzo cha kulipiza kisasi kilichosababisha mauaji ya Tupac saa chache baadaye.
Kwa mujibu wa mashtaka, Keffe D alihusika katika kupanga shambulio hilo na kutoa silaha iliyotumika, ingawa hakutuhumiwa kuwa ndiye aliyempiga Tupac risasi moja kwa moja.
Kauli zake zamgeukia
Kesi hiyo ilibaki bila jibu kwa miongo kadhaa hadi jina la Keffe D lilipoanza kuibuka tena kutokana na maelezo aliyokuwa ameyatoa mwenyewe katika mahojiano mbalimbali pamoja na kitabu chake cha mwaka 2019, Compton Street Legend.
Waendesha mashtaka walitumia baadhi ya kauli hizo kama ushahidi katika kesi hiyo, wakidai kuwa Davis alikuwa amezungumza kuhusu nafasi yake katika tukio hilo.
Kesi ilianza rasmi kusikilizwa mahakamani Agosti 17, 2026, ikiwa ni takribani miaka 30 baada ya mauaji hayo.
Katika upande wa utetezi, wakili wa Keffe D, Michael Sanft, alijaribu kupunguza uzito wa kauli za mteja wake, akidai kuwa Davis alikuwa mtu anayependa kusimulia hadithi na kuongeza chumvi katika maelezo yake. Hata hivyo, majaji walifikia uamuzi wa kumtia hatiani baada ya kusikiliza ushahidi uliowasilishwa katika kipindi cha kesi.
Anakabiliwa na kifungo cha maisha
Baada ya kupatikana na hatia, Keffe D sasa anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa kifungo cha maisha jela. Kwa sasa anaendelea kushikiliwa bila dhamana.
Ripoti ya PEOPLE imesema Davis tayari amemweleza jaji kuwa anapanga kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.